.

.

.

.

Sunday

PASTOR CARLOS KIRIMBAI: USIJIKINAI NA KUJIONA WEWE NDO UPO SAWA NA WENGINE WOTE WAMEKOSEA

Pastor Carlos Ricky Wilson Kirimbai
Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa. (LK. 18:9-14 SUV).

Nafurahishwa sana ninapouona utofauti uliyopo kwenye Mwili wa Yesu Kristo. Mungu anaweka kwa watu tofauti namna tofauti ya kufanya kazi Yake na kuufikisha ujumbe wa Ufalme wa Mungu kwa watu na makundi mbali mbali ya watu.

Yaani inapendeza mno kuona diversity iliyopo kwenye mwili wa Kristo.

Kinachonisumbua sana ni pale mmoja wetu anapojiona yeye ndo yupo sawa na wengine wote wameingia chaka. Tunapojiona sisi ndo tupo kiroho na wengine wote wapo kimwili au wapo kidini.

Hivi hakuna namna ambayo kila mmoja wetu anaweza akafanya kazi ya Mungu kwa namna alivyowekewa ndani kuifanya na kwa neema na upako ambao upo juu yake bila ya kuwasema wengine ambao wanafanya tofauti na tunavyofanya sisi na ambao wameitwa na Mungu kuyafikia makundi tofauti ya watu?

Hivi ni kweli kuwa ni sisi tu ndo tupo sahihi na wengine wote hawapo sahihi?

Unashawishika kabisa kuwa ufanyavyo wewe ndo sahihi kuliko wengine wote?

Je ni kweli Mungu alipokuja akakuita alikuambia nenda kaifanye kazi yangu kwa sababu hakuna mwingine anaifanya?

Nini mantiki sasa ya maneno ya Yesu kuwa mavuno ni mengi na watenda kazi ni wachache kama unafikiri ni wewe na kakundi kako kadogo ka watu peke yenu ndo mpo sahihi?

Hivi kweli unadhani na hako kakundi ka makumi, au mamia, au maelfu ya watu tu miongoni mwa Watanzania millioni 45 na zaidi ndo mpo sahihi na ndo nyie tu Yesu anaridhika nanyi kwenda Kwake?

Inakuwaje unajiona wewe ndo upo kiroho na wengine wote wapo kimwili, kidini, kisheria sana?

Una uhakika kuwa hivyo unavyowaza ndivyo mwenye kazi Naye ana waza hivyo?

Style yako ya kufanya huduma nani amekuambia ndo sahihi kuliko zote alafu wengine wote wana style isiyo sahihi?

Nilidhani kuwa style hiyo ni sahihi kwa kundi la watu ambao umeitwa kuwafikia na sio kila mtu anafikiwa kwa style moja tu.

Kwani kazi ya kufikia watu si inafananishwa na uvuvi?

Je samaki wote wanavuliwa kwa mtindo mmoja?

Kazi ya kuwafikia watu inafananishwa na uvunaji.

Je uvunaji wote unafanyika kwa mtindo mmoja?

Kwanini tunakuwa watoto hivi?

Huwa nina admire sana kazi ambazo wanazifanya watumishi na huduma mbalimbali ila kweli ninapata shida pale wanapoanza kuwasema wengine na kuwaona hawafanyi kwa kiwango.

Umeitwa upime kazi za watu au ufanye wewe kile ulichoitwa ufanye?

Hivi macho yanaweza kweli kupima kazi ya mtu?

Nikisoma maandiko neno la Mungu linasema kazi ya kila mmoja itajaribiwa kwa moto!

Si tungoje tu kazi zetu hizi zije zijaribiwe kwa moto ndipo tutajua zilikuwa kazi za namna gani?

Style yangu sio kwamba ni sawa na ya kwako si sawa bali ni sawa katika mazingira niliyoitiwa na kwa watu niliyokusudiwa kuwafikia. Siwezi kufanya kama wewe na wewe huwezi kufanya kama mimi.

Kila mtu afanye kwa zamu yake bila kupondana na kusagiana.

Kila mtu akimbie mbio kwenye safu yake. Tusisukumane na tusiingiliane kwenye safu.

Neema ya Mungu ipo juu ya kila mmoja wetu kufanya vile tulivyoitwa na Mungu kufanya.

Tuache kujiona sahihi kuliko wengine maana huo sasa ndo udini na ufarisayo wa hali ya juu.

Tuache kujikinai na kujihesabia haki huku tukidharau wengine wote.

No comments:

Post a Comment