.

.

.

.

Friday

YESU ANAKUSAIDIAJE KUKABILIANA NA MAPITO NA MAGUMU YA MAISHA.

Kama pamoja na kwamba umeokoka lakini mapito ya maisha yanakudhoofisha, kukunyong'onyesha, kukufadhaisha na kukukatisha tamaa kama vile yanavyomfanya mtu ambaye hajaokoka na hana Yesu ndani yake, basi hujajua jinsi ya kutembea na Yesu katika uhalisia wa maisha ya kila siku ya hapa duniani yaliyojaa changamoto.

Maandiko yanasema:
I Yohana 4: 4.

4Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.

Hata uwe mtoto mdogo vipi kiroho, kumbuka unatokana na Mungu na umekwisha shinda kila shida, adha, changamoto na mateso maishani mwako maana Aliye ndani yako ni mkuu kuliko aliye katika dunia.

Yesu hakusaidii toka mbinguni bali anakusaidia toka ndani yako.
Yupo ndani yako.

Usisahau kuwa ulimpokea maishani mwako aje akae ndani yako.
Yesu ni zaidi ya msaada uliyo karibu upatikanao tele wakati wa mateso, shida, adha na mateso.
Lakini ili ushinde maishani lazima uwe na imani katika Yeye uliyembeba ndani.

Maandiko yanasema:
I Yohana 5: 4.

4Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu.

Mimi na wewe tumezaliwa na Mungu na kwa hiyo tunaushinda ulimwengu na shida zake, adha zake, mateso yake na changamoto zake.

Lakini ukumbuke kuwa kinachoushinda ulimwengu ni hiyo imani yetu.
Imani yako ikidhoofika na kutindika, shida adha, mateso, changamoto na mapito ya maisha yatakuzidi nguvu na utashuka moyo, kufadhaika na kupata msongo wa mawazo.
Furaha na amani yako vitaibiwa.

Yesu aliwaambia wanafunzi Wake na Petro:
Luka 22: 31, 32.
31 Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; 32lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.
Katika mapito mbali mbali ya maisha ni muhimu sana kulinda imani yako isitindike.
Linda sana unawaza nini katika mapito yako.
Je unawaza sawa na neno la Mungu linavyosema au unawaza sawa na shetani na mazingira yako wanavyosema.

Unajua kuwa unamsikiliza shetani na mazingira yako kwa sababu ya matokeo ambayo unayoana maishani mwako.

Ukiona unavutwa chini na nafsi yako inainamishwa basi ujue unamsikiliza shetani na mahubiri yake kichwani mwako.

Maandiko yanasema:
Isaya 26: 3.
3Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea
Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini.
Ukiona tu hakuna amani kamilifu maishani mwako basi ujue moyo wako haumtegemei Mungu hata kidogo na tumaini lako Kwake limefifishwa na adui.

Daudi alisema:
Zaburi 16: 8.
8 Nimemweka BWANA mbele yangu daima,
Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa.
Nini unakiweka mbele yako daima?
Je ni mapito yako?
Shida zako?
Mashaka yako?
Adha zako?

Ndiyo maana ni rahisi sana kuondoshwa maana umeamua kwa hiari yako kuviweka vingine mbele yako isipokuwa Bwana.

Bwana akiwa mbele yako, ukamwona Yeye na ahadi zake kwako, haijalishi nini unapitia, hutaondoshwa kamwe.

Adui anaporusha mishale yenye moto, mishale hiyo ipo katika sura ya mawazo ya kukukatisha tamaa, kukunyong'onyesha, kukuinamisha nafsi, kukutazamisha mapungufu na madhaifu yako nk.
Usipokuwa na imani hutakuwa na kinga dhidi ya mashambulio hayo.
Mishale itapenya na kukudhuru nafsini mwako na unajua kuwa nafsi yako imedhurika na mishale ya adui kwa jinsi unavyowaza, maamuzi yako ya ajabu ajabu na hisia zako ambazo hazina utulivu hususa kusikitika, kushuka moyo, kukata tamaa, kusononeka, msongo wa mawazo nk.

Dawa ya hivi ipo kwako.
Imani yako.
Zaidi ya yote twaeni ngao ya imani ambayo kwa hiyo mtaizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.

Imani haizimi baadhi ya ishale yenye moto ya adui.
Inaizima yote.
Inainyanganya nguvu ya kukudhuru.
Ukiona kuna madhara, shida ni imani yako ni mswaki.
Ifanyie kazi imani yako.

Unapopita katika mapito mbali mbali, sio kile Mungu anafanya ndicho kitakuvusha, bali ni kile ambacho unafanya wewe kushirikiana na kile ambacho Mungu ameshafanya ndicho kitakuvusha.
Mungu anatupa kushinda na zaidi ya kushinda kwa njia yake Yeye aliyetupenda.
Sasa kama unashinda au la maishani mwako haimtegemei tena Mungu inakutegemea zaidi wewe unafanya nini na kile ambacho Mungu ameshafanya.

Yesu anatushangiliza daima na anasababisha manukato ya harufu ya kumjua Yeye idhihirike kila mahali kwa kazi zetu.

Sio Yeye ni wewe unafanya nini na kile ambacho Yeye ameshafanya.
Umeokoka.

Acha kuteswa na mambo yale yale yanayowatesa watu wasio na Yesu.
Kila mtu anapata shida, adha, mateso, maumivu, changamoto na mambo yanayofanana na hayo maishani.

Ila sio kila mtu ana Mungu nan ahadi Zake maishani mwake.
Ukiona wengine wana furaha sio kwamba hawana hayo ila wamejua jinsi ya kuishi nayo pasipo kuyaruhusu yawaathiri na kuwanyang'anya raha na amani yao katika Mungu.
Upo chini kwa sababu umekubali kuwa chini.

Utanyanyuka toka hapo ulipo kwa sababu umeamua kufanya hivyo.
Kila hali hubaki vile vile ilivyo isipokuwa mtu ameamua kusababisha badiliko.
Nimalize na maneno haya ya Mfalme Daudi:
Zaburi 42: 5 - 11.
5 Nafsi yangu, kwa nini kuinama,
Na kufadhaika ndani yangu?
Umtumaini Mungu;
Kwa maana nitakuja kumsifu,
Aliye afya ya uso wangu,
Na Mungu wangu.
6Nafsi yangu imeinama ndani yangu, kwa hiyo nitakukumbuka,
Toka nchi ya Yordani, na Mahermoni, na toka kilima cha Mizari.
7 Kilindi chapigia kelele kilindi kwa sauti ya maboromoko ya maji yako,
Gharika zako zote na mawimbi yako yote yamepita juu yangu.
8 Mchana BWANA ataagiza fadhili zake, na usiku wimbo wake utakuwa nami,
Naam, maombi kwa Mungu aliye uhai wangu.
9Nitamwambia Mungu, mwamba wangu, Kwa nini umenisahau?
Kwa nini ninakwenda nikihuzunika, adui wakinionea?
10Watesi wangu hunitukana mithili ya kuniponda mifupa yangu,
Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako?
11Nafsi yangu, kwa nini kuinama,
Na kufadhaika ndani yangu?
Umtumaini Mungu;
Kwa maana nitakuja kumsifu,
Aliye afya ya uso wangu,
Na Mungu wangu.
Uamuzi ni wako.
Endelea kuinamishwa nafsi au amua kunyanyuka na kufurahia maisha.
Acha kuruhusu nafsi yako kukusemesha.
Wewe isemeshe kama Daudi alivyoisemesha.

NEEMA NA AMANI ZIZIDISHWE KWAKO KATIKA KUMJUA BWANA NA MWOKOZI WETU YESU KRISTO.

Imeandaliwa na Mchungaji Carlos Ricky Wilson Kirimbai - Facebook Page

No comments:

Post a Comment