.

.

.

.

Monday

YUPO MALAIKA MWENYE GUDULIA LAKO LA MAJI NA MKATE ULIYOOKWA KWENYE MAKAA.

Pastor Caros Kilimbai wa Manna Tabernacle Ministry
Mpendwa wangu haijalishi umepakwa mafuta kiasi gani na upo gifted kiasi gani, maishani mwako utahitaji hawa watu waliyo Malaika wenye gudulia la maji yatokayo juu ili kukunywesha na mkate uliyookwa kwenye makaa ya moto ili kukulisha.

Malaika hawa ni watu waliyopakwa mafuta na Mungu kama viongozi wa kiroho, wachungaji watakao kuongoza kando ya maji ya utulivu na kukulaza katika malisho ya majani mabichi.

Hata upakwe mafuta vipi, hata uwe gifted vipi usije ukafanya kosa la kudhani kuwa hutahitaji Mchungaji. Usijidanganye kudhani kuwa maishani you will make it alone bila wao tena hata siku moja usifanye kosa la kudhani hawa watu sio wa muhimu na hutawahitaji.

Kwenye kitabu cha Ufunuo wa Yohana, mara saba Yesu anamwagiza Yohona aandike kwa Malaika wa Kanisa husika ambalo anataka kusema nalo.

Roho Mtakatifu yupo na Mungu husema na watu Wake moja kwa moja kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Lakini yapo mambo Mungu hatasema nawe moja kwa moja bali kupitia Malaika wa Kanisa ulilopo. 

Huyu Malaika ni mwanadamu kama wewe na mimi ambaye ni kiongozi wa kanisa ambaye huwa tunamjua kama Mchungaji.

Wale Malaika saba wa makanisa saba ya kitabu cha Ufunuo walikuwa wanadamu kama mimi na wewe ambao waliwekwa na Mungu kama viongozi juu ya yale makanisa.

Malaika wa Kanisa fulani ni set man juu ya ile local gathering ya believers aliyewekwa hapo na Mungu na yapo maonyo na maelekezo ambayo Mungu huyaleta kwa waliyo kanisani humo kupitia yeye.

Kila mtu anahitaji kanisa, yaani mkusanyiko wa waamini ambao unawekwa na Mungu chini ya Mchungaji wa mahali ili kulishwa nae ufahamu na maarifa.

Katika siku zetu hizi tuna watu wengi mno ambao hawana kusanyiko la waamini ambalo wao ni sehemu ya hilo kwa hiyo hawana Mchungaji au Malaika. Hii ni hatari sana kama tutakavyoona muda sio mrefu.

Sasa kabla hatujaendelea mbali tuone maana ya hili neno Malaika ili itusaidie kuona jinsi ambavyo hawa Wachungaji wetu walivyo Malaika.

Neno Malaika linatokana na neno la lugha ya asili Angelos ambalo linamaanisha Mjumbe au aliyetumwa.

Mchungaji Wako ni Mjumbe wa Bwana wa Majeshi kwa watu waliyo kwenye kusanyiko la waamini ambalo amewekwa juu yao.

Maandiko yanatuambia:

AYU. 33:23 SUV

Kwamba akiwapo malaika pamoja naye, Mkalimani, mmoja katika elfu, Ili kumwonyesha binadamu hayo yampasayo;

Hapa anatuambia kwamba akiwapo malaika, mwanadamu, mjumbe wa Bwana wa Majeshi.

Huyu malaika ni Mkalimani. Mkalimani ni mtu anayetufanya tuelewe lugha iliyo ngeni kwetu kwa kutumia lugha ambayo sisi tunaielewa. Anachukua maneno yaliyo kwenye lugha tusiyoielewa na kuyaweka katika lugha ambayo mimi na wewe tunaweza kuielewa.

Lugha ya maandiko ipo kiroho sana na kuna maeneo mengi ya maandiko yana maelekezo kwetu ambayo yanahitaji Mkalimani kuyatafsiri kwa lugha nyepesi ya kawaida ya kila siku ambayo mimi na wewe tunaielewa ili tujue yatupasayo.

Bila huyu Mkalimani hutayajua yakupasayo kwa hiyo hutafanya yakupasayo na matokeo yake hutapata yakustahiliyo.

Eliya Mtishbi kuna wakati alifikwa na mambo magumu sana na pamoja na kwamba alikuwa amepakwa sana mafuta alihitaji huduma ya malaika mwenye gudulia la maji na mkate uliyookwa kwenye makaa.

Pamoja na kwamba alishusha moto juu ya Mlima Karmeli na kuua manabii 400 wa Baali na 450 wa maAshera lakini Yezebeli alitishia kumwua akakimbilia jangwani na akiwa huko akatamani kufa.

Huduma ya malaika ikawa ndo msaada wake.

1 FAL. 19:3-8 SUV

Naye alipoona hayo, aliondoka, akaenda aihifadhi roho yake, akafika Beer-sheba, mji wa Yuda, akamwacha mtumishi wake huko. Lakini yeye mwenyewe akaendelea katika jangwa mwendo wa siku moja, akaenda akaketi chini ya mretemu. Akajiombea roho yake afe, akasema, Yatosha; sasa, Ee BWANA, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu. Naye akajinyosha akalala chini ya mretemu; na tazama, malaika akamgusa, akamwambia, Inuka, ule. Akatazama, kumbe! Pana mkate umeokwa juu ya makaa, na gudulia la maji, kichwani pake. Akala, akanywa, akajinyosha tena. Malaika wa BWANA akamwendea mara ya pili, akamgusa, akasema, Inuka, ule; maana safari hii ni kubwa mno kwako. Akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu, mlima wa Mungu.

Akiwa amekimbilia jangwani tena akiwa chini ya mti wa Mretemu akijiombea nafsi yake afe, malaika alimgusa akamwambia ainuke #ale.

Huna Mchungaji unakulaje kwa mfano?

Tena maandiko yanasema wazi

YER. 3:15 SUV

nami nitawapa ninyi wachungaji wanipendezao moyo wangu, #watakaowalisha kwa maarifa na fahamu.

Sasa kama huna Mchungaji unalishwaje kwa mfano?

Unaweza kudhani kuwa huhitaji kulishwa wewe. Unaweza kula tu peke yako. Hii ni imani isiyo na msingi wowote katika maandiko.

Kama tusingehitaji kulishwa kwanini Yesu amwambie Petro Lisha kondoo zangu. Kama wanaweza kula wenyewe walishwe ya nini hasa?

YN. 21:15-17 SUV

Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, #Lisha wana-kondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, #Lisha kondoo zangu.

Tena kwenye hii mistari anazungumzia kuhusu kulisha kondoo (wapendwa waliyokomaa kiroho) na wana kondoo (wapendwa waliyo wachanga kiroho).

Hapatawahi kutokea wakati wowote katika maisha yako ambayo hutahitaji Mchungaji. Kama unajiona huhitaji mchungaji hiyo ni moja ya dalili za umevurugwa kiasi gani.

Pale Eliya ndo alikuwa anakufa lakini asante Yesu akaamshwa ili ale.

Alipoamka akakuta mkate uliyookwa juu ya makaa na gudulia la maji.

Ukisoma neno la Mungu unakutana na mkate wa uzima. Ukifundishwa na hawa Malaika, wakalimani unapata mkate uliyookwa juu ya makaa. Neno ambalo limejaribiwa kwenye maisha yao wenyewe kupitia mapito yao na Bwana. Fundisho linalokutoa mahali kukupeleka mahali.

Gudulia la maji ni maneno ya kukutia moyo, kukufariji na kukutia nguvu kutoka kwa hawa malaika, wakalimani.

Alipokula na kunywa mara ya kwanza ilimtoa katika ile hali ya kutaka kufa.

Akaguswa tena akala na kunywa tena akaenda kwa nguvu ya chakuka kile siku 40.

Kuna umbali katika kipawa chako, karama yako, huduma yako, upako wako na hata maishani mwako ambao huwezi kwenda bila ya kula mkate uliyookwa kwenye makaa na kunywa maji toka kwenye gudulia. 

Kubali ukatae, elewa usielewe, unamhitaji malaika, mkalimani, moja katika elfu awe anakuambia yakupasayo.

Kama hunaye huyu hutaenda mbali.

No comments:

Post a Comment