.

.

.

.

Friday

Mwingulu:Maaskofu, Masheikh wananitaka urais 2015

Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, amesema makundi mbalimbali ya kijamii yameomuomba agombee urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.

Nchemba, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, aliyataja makundi hayo kuwa ni pamoja na viongozi wa dini ya Kiislamu na Kikristo, wanafunzi wa vyuo vikuu, Watanzania wanaoishi nje ya nchi, wakulima na hadi watu wa vijiweni.

“Hata hivi karibuni nilipoenda Mwanza nilikuta bango kubwa limeandikwa ‘Mwigulu ni wewe unayekuja, au tumsubiri mwingine?” alisema wakati akihojiwa na kituo cha redio cha jijini Dar es Salaam jana asubuhi.

“Ujumbe kama huu wa ‘ni wewe unayekuja, au tumsubiri mwingine’ alipewa bwana mkubwa Yesu zama hizo. Aliulizwa na watu wake, akawajibu ‘mkiona neema zinakuja mjue ndivyo’.”

Hata hivyo, Mwigulu alipotakiwa kutoa kauli yake kama atagombea, hakutaka kukubali wala kukataa na badala yake akachukua fursa hiyo kuwashukuru wale wote ambao wamekuwa wakimtumia ujumbe wa kumtaka agombee.

Na alipobanwa zaidi, alisema: “Tutajua kama tutavuka mto tutakapofika mtoni.”

Hata hivyo, akizungumza jana mchana na waandishi wa habari katika Hospitali ya Mwananyamala, alisema kwa sasa hawezi kusema kama atagombea ama la kutokana na majukumu aliyopewa na Rais Jakaya Kikwete.

Alisema jukumu la kwanza alilopewa ni kusimamia Wizara ya Fedha ambayo jukumu kubwa ni kuhakikisha kodi zote zinakusanywa na kuwafikia Watanzania kwa usawa.

Alisema jukumu lingine ni la Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho yeye ni Naibu Katibu Mkuu Bara na kwamba anategemewa kutimiza majukumu aliyopewa ya kichama.

Nchemba hata hivyo, alisema kuwa atatoa  maamuzi yake ya kugombea ama la kipenga kitakapopulizwa akimaanisha muda rasmi CCM kitakapotangaza kuanza mchakato wa uteuzi wa mgombea.

Kwa miezi kadhaa sasa, Mwigulu amekuwa akitajwa kuwa miongoni mwa makada wa CCM watakaojitosa katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya kuwa mgombea wa urais kupitia chama hicho tawala ili kurithi nafasi itakayoachwa wazi na Rais Kikwete anayetarajiwa kumaliza kipindi chake cha uongozi cha miaka 10 mwishoni mwa mwaka huu.

Wengine wanaohusishwa na harakati za kuwania nafasi hiyo ni mawaziri wakuu wastaafu, Fredrick Sumaye na Edward Lowassa; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja;  Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha-Rose Migiro.

Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalah, walishatangaza nia ya kujitosa kwenye mbio za kuwania urais wakiwa ziarani nchini Uingereza huku Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Singida Kaskazini,  Lazaro Nyalandu akitangaza nia hiyo mwezi uliopita wakati akihutubia mkutano wa hadhara jimboni kwake. Dk.

Kigwangalah, alitangaza nia yake ya kujitosa kwenye mbio za urais wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

WAKWEPA KODI
Katika hatua nyingine, Mwigulu alisema anataka kuona watu ambao wanakwepa kulipa kodi na wakathibitika kutolipa kodi wanafungwa gerezani ili iwe somo kwa wengine.

Alisema anayekwepa kulipa kodi ni muuaji kwa sababu kuna watu wanakosa dawa na wanakufa kwa sababu ya ukwepaji wake huo.

“Kama mtu amekwepa kulipa kodi na ikathibitika kwamba amekwepa afungwe gerezani. Hapaswi kuwapo nje kwa sababu akiwa nje atahonga.
Anatakiwa alipe kodi na kisha akakae gerezani.

“Hatuwezi kufukuzana na mama mjane, huyu ambaye anauza karanga ili amsomeshe mwanaye ili tupate kodi ya senti chache wakati tunawaachia watu ambao wanakwepa kulipa mabilioni ya kodi,” alisema.

Aliongeza kuwa hakubaliani na utaratibu wa kuwaondoa kwenye nafasi zao watu wasio na uzalendo wa nchi yao na kuwaacha huru hata baada ya kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya fedha (kama bilioni 30); na badala yake akasema anataka watu hao wapelekwe gerezani kwani kutochukua hatua kali dhidi yao kunawapa nafasi ya kwenda kutumia vizuri fedha nyingi walizohujumu.

“Inapotokea kodi inayopaswa kulipwa ni dola milioni 45, halafu afisa wa kodi anaandika kiasi kinachotakiwa kulipwa kuwa ni Sh. milioni 45, huyu lazima ashughulikiwe kwa sababu lazima kuna tatizo. Haiwezekani afisa wa mamlaka ya kodi awe hajui kutofautisha kati ya Dola na Shilingi. Lazima ashughulikiwe. Na kama ni kweli kwamba hajui kutofautisha dola na shilingi, hafai kuwapo ofisini,” alisema.

Aidha Mwigulu alisema hivi sasa anaendelea na mapambano dhidi ya watumishi wa umma wanaolipa mishahara hewa.

“Nilipata upinzani kidogo hapa kutoka kwa watu wanaonufaika na jambo hili, wakitoa sababu nyepesi kwamba ni ngumu kujua viwango vya michango yao katika mifuko mbalimbali na madeni mengine yanayowakabili. Lakini nasema kwamba mwajiri atakata michango yote kisha mishahara ndiyo italipwa kwa wahusika halali tu,” alisema.



CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment