.

.

.

.

Tuesday

Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Bilal awaangukia viongozi wa Dini urais 2015


Viongozi wa dini nchini,  wametakiwa kuwakemea wanasiasa na watu wote wanaotaka kuingia madarakani kupitia migongo ya wanyonge kwa manufaa yao binafsi.

 Kauli hiyo ilitolewa jana, mjini hapa na Makamu wa Rais,  Dk. Mohamed Gharib Bilal, katika ibada ya kumsimika Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dodoma, Mhashamu Askofu Beatus Kinyaiya.

Bilal alisema ni vema wakakumbuka kigezo kikubwa cha kiongozi bora ni yule mwenye hofu ya Mungu na anaewajali watu anaowaongoza bila ubaguzi wowote.

“Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa viongozi katika ngazi mbalimbali, chaguzi hizi zimekuwa zikiibua hisia tofauti miongoni mwa wananchi, nitumie nafasi hii kuwaomba viongozi wa dini zote nchini kuliombea Taifa letu katika kipindi hiki ili wananchi waweze kufanya uamuzi sahihi,” alisema Dk. Bilal.

Alibainisha kuwa uamuzi huo utawafanya kuchagua watu ambao wataliongoza Taifa kwa kuendeleza misingi ya amani, umoja, upendo na mshikamano.
“Napenda niwahakikishie kwamba, Serikali yenu imejipanga vilivyo kuhakikisha inasimamia zoezi lote la uchaguzi kwa misingi ya haki, amani na utulivu, tunaamini zoezi hilo litafanyika kwa amani na utulivu mkubwa na mwisho wa siku Watanzania watapata viongozi wazuri, wanaowataka ili washirikiane nao kusukuma mbele gurudumu la maendeleo yetu,” alisema Dk. Bilal.
Makamu wa Rais,  Dk. Mohamed

 Akizungumzia amani, Dk. Bilal aliwataka Watanzania kudumisha amani, umoja, upendo na mshikamano wa Taifa.

 “Mungu ameibariki sana nchi yetu, tumeishi kwa muda mrefu kama Taifa moja lenye amani na mshikamano mkubwa bila kujali tofauti za rangi, kabila, dini wala hali za watu, amani ni sharti la kwanza katika maendeleo ya binadamu,” alisema Dk. Bilal.

 Aidha, alisema kuna watu wanadhani wanapozungumzia kulinda amani ya nchi ni hila za siasa tu, na kwamba wanaosema hivyo wamepotoka wapuuzwe na kuwaombea kama alivyosema Yesu Kristu pale msalabani.

“Ni nadra sana kukuta jambo hili katika nchi zingine, wote ni mashahidi, tunasikia kila siku kupitia vyombo vya habari namna wenzetu wanavyoishi, ni maisha ya hofu, taabu na mateso makubwa, haya yote yanatokana na kukosa amani…amani tunayoizungumza si lugha ya wanasiasa,” alisisitiza Dk. Bilal. 

Aliwataka viongozi wa dini zote kuombea upendo ndani ya jamii, watu wapendane waishi bila chuki, bila ubinafsi, wasameheane pale panapotokea mikwaruzano ili amani iendelee kustawi.

Dk. Bilal alilipongeza Kanisa Katoliki nchini kwa mchango wake mkubwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali kuwaletea wananchi maendeleo na kupambana na umaskini.

“Mbali ya malengo ya kuwajenga watu kiroho, Kanisa Katoliki na taasisi zake limekuwa mdau muhimu wa Serikali katika kuimarisha huduma mbalimbali za jamii katika nyanja za elimu, afya, maji, kilimo, utunzaji na uboreshaji mazingira,” alisema Dk. Bilal.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa kwanza wa jimbo hilo, Kinyaiya, aliwataka wazazi kutimiza wajibu wao katika kusimamia maadili ya watoto wao ili kupunguza mmonyoko wa maadili katika jamii.

Alisema kama wazazi watasimamia ipasavyo maadili, hakutakuwa na makundi ya kihalifu kama ‘Panya road’ na mengine yakiwamo ya wanywa viroba na waendesha bodaboda ‘rafu’  pamoja na watumiaji wa dawa za kulevya.

 Aidha, aliitaka jamii kuwa mstari wa mbele kutunza mazingira na rasilimali zake kama vile wanyamapori hasa tembo ambao wako mbioni kutoweka kutokana na kuuawa kwa wingi kwa biashara haramu ya meno yake.

“Wenzetu walishafanya makosa kama tunavyofanya hivi sasa kwa kuwaua tembo hali ambayo imewapelekea wao kusafiri umbali mrefu kuja kuangalia wanyama kama vivutio vya utalii,” alisema Kinyaiya.

Aliitaka jamii iishi kwa kuitunza na kuilinda amani iliyopo kwa kuacha kujihusisha na mambo yanayochangia kutoweka kwa amani nchini.

Jimbo la Dodoma lilipewa hadhi ya kuwa Jimbo  Kuu mwishoni mwa mwaka jana na linakuwa la sita nchini.

Majimbo mengine makuu ni Arusha, Dar es Salaam, Tabora, Songea na Mwanza.

Viongozi waliohudhuria sherehe hizo ni pamoja na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na Mkewe Anna Mkapa; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi; Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe; Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa.

 Wengine ni  Balozi wa Papa nchini, Askofu Mkuu Francesco Padilla; Maaskofu wa kanisa hilo wakiongozwa na Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na viongozi wengine wa Serikali.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment