.

.

.

.

Tuesday

Askofu: Chanzo Panya Road ukosefu wa ajira

Askofu mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Frederick Shoo, amesema taifa kwa sasa linakabiliwa na changamoto nyingi, hali ambayo inawakatisha tamaa vijana kukabiliana na makali ya maisha na ukosefu wa ajira na kuonya kama hazitapatiwa ufumbuzi, kuna uwezekano mkubwa ‘Panya Road’ wakasambaa nchini kote.

Amezitaja changamoto ambazo zinalikabili taifa kuwa ni sekta za afya, elimu na kilimo.

Aliyasema hayo katika ibada maalum ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwake (Askofu Dk. Shoo) kuchukua nafasi ya mtangulizi wake, Askofu Dk. Martin Shao, aliyestaafu. 

“Hali ikiendelea hivi, ni hatari kwa taifa letu, kwa sababu watu waliokata tamaa hawatawaliki na ikiendelea hivi tusishangae kuona ‘Panya Road’ wakitokea hata hapa kwetu Kilimanjaro na kwingineko pia...ni lazima tuchukue hatua,” alisema Dk. Shoo.

‘Panya Road’ ni kundi la vijana linalodhaniwa kuwa ni la kihalifu, ambalo wiki chache zilizopita lilitoa hofu kubwa kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, yakiwamo maeneo ya Tandale, Manzese, Magomeni, Mabibo na mengineyo.

Kundi hilo lilizua hofu na kusababisha maduka kufungwa mapema, huku watu wakikimbia ovyo kwa hofu na shughuli zote kwenye baadhi ya maeneo ya Jiji kusimama mpaka pale hali ilipotengemaa.

Baadhi ya maeneo, kama vile Magomeni, Tabata, Kinondoni na kwingineko, kundi hilo lililiripotiwa kupita na kufanya uhalifu, ikiwamo kupora watembea kwa miguu, madukani na kukaba.

Vitendo hivyo vilifanywa na kundi hilo baada ya kutoka makaburini kumzika mwenzao anayedaiwa kuuawa na polisi, ndipo walipoamua kulipiza kisasi kwa kufanya fujo hizo.

Kuhusu kushuka kwa ubora katika huduma ya elimu na afya, Dk. Shoo alisema kwa sasa elimu bora na huduma bora ya matibabu anayezipata lazima awe tajiri.

“Viongozi wetu kusema kwamba nchi yetu ni maskini na kuamini hivyo, huo ni umaskini wa fikra,” alisema Dk. Shoo. 

Aliongeza: “Hali kadhalika, umaskini wa wengi hapa nchini imekuwa kama kuhukumiwa kifo. Tunachohitaji ni viongozi na watumishi wenye roho ya uzalendo…bila hivyo ni vigumu sana kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi hii zinawanufaisha Watanzania wote.”

Ibada hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Kapteni mstaafu, George Mkuchika, aliyemwakilisha Rais Jakaya Kikwete. 

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment