.

.

.

.

Saturday

Viongozi wa Dini walaani, wasema hofu ya Mungu imeondoka

Viongozi wa dini wamesema vitendo vya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi vinasababishwa na baadhi ya wanasiasa kuamini ushirikina badala ya Mungu.
Kauli ya viongozi hao imekuja baada ya kushamiri kwa matukio hayo hasa kipindi cha uchaguzi.

Wiki iliyopita mtoto Yohana Bahati  mwenye umri wa mwaka mmoja aliporwa na wauaji kutoka mgongoni kwa mama yake na kwenda kunyofolewa mikono na miguu kisha mwili wake kufukiwa katika pori la Hifadhi ya Biharamulo lililoko Wilaya ya Biharamulo, Mkoa wa Kagera.

Wakizungumza na  chanzo cha habari hii  Jumamosi kwa nyakati tofauti, viongozi hao wameonyesha wasiwasi kuwa inawezekana baadhi ya wanasiasa huwatafuta waganga ambao huwatuma viungo vya binadamu ili wafanikiwe kwenye nafasi mbalimbali wanazogombea kwenye nchi.

Kiongozi wa Dini ya kiislam Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Mussa Salum, alisema kuwa mauaji hayo ni zaidi ya mmomonyoko wa maadili na kwamba ni ukatili uliosababishwa na roho mbaya.

“Lazima kama nchi bila kujali wewe ni kiongozi wa dini, mwanasiasa wenye hofu ya Mungu tusimame pamoja tuwataje wauaji hawa kwa kuwa tupo nao kwenye jamii zetu,” alisema.
Alisema baadhi ya wanasiasa wanaoamini ushirikina wanachangia kuwapo kwa vitendo hivi vya kinyama.

“Viongozi wa aina hii ni wa kuogopwa ni watu hatari sana, tunahitaji nguvu ya pamoja kuwaibua,” alisema.

Kuhusu waganga Sheikh Salum aliitaka Serikali iweke utaratibu wa kuwachunguza watu hao kujua wanatoka wapi na asili zao.
Alisema ipo haja ya viongozi wa dini sasa kukaa pamoja ili kuisaidia serikali katika kutokomeza vitendo hivyo.

Mchungaji John Kamoyo kutoka Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT),  alisema kwa sasa upo ushirikina mwingi katika taifa ambao unahitaji nguvu ya pamoja ya viongozi wa dini kuuondoa.

“Watu wanaamini watapata utajiri kwa ushirikina, hii ipo kwa wenye elimu na wasiokuwa nayo, wanadanganywa na  waganga ili wapandishwe vyeo au kupata nafasi wanazogombea,” alisema.

Aliongeza kuwa, baadhi ya viongozi waliopo madarakani wakiachana na imani hii itasaidia kupunguza tatizo la mauaji ya watu hawa.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekoste Tanzania, William Mwamalanga,  alisema kuwa vitendo hivyo vinaleta taswira mbaya ndani ya nchi na kimataifa.

Alisema serikali inatakiwa kujitathmini kuhusu matukio ya ushirikina ambayo ni chukizo mbele ya Mungu.

Alipendekeza serikali iandae kura ya siri ambayo itakuwa ikipigwa kabla ya uchaguzi itakayowezesha wananchi kuwataja wale wote wanaohusika na mauaji hayo.

Alisema kwa kufanya hivyo itasaidia kupata viongozi bora wenye sifa ambao hawatatokana na umwagaji damu za watu.

Aidha, alisema Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, licha ya kutangaza marufuku mabango ya waganga lakini bado yamezagaa maeneo tofauti nchini.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment