Wakati mvutano wa rasimu ya kanuni za Bunge Maalum la Katiba juu ya njia ya upigaji kura ama ya siri au ya dhahiri ukizidi kuligawa Bunge, Tamko la Kanisa Katoliki juu ya muundo wa Rasimu ya Katiba limesambazwa kwa baadhi ya wabunge likiasa kuwa umakini unatakiwa kutamalaki katika kupitisha katiba mpya.
Tamko hilo wenye kurasa 15 ambalo limeandikwa kitaalamu liliandaliwa na Tume ya Haki na Amani la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanznia (Tec), na Wanataaluma Wakristo Tanzania (CPT).
Paulo Ruzoka |
Tamko hilo linaasa Bunge Maalum la Katiba juu Rasimu ya Katiba likilitaka kutokashifu mapendekezo ya serikali tatu kama yalivyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwenye rasimu ya kwanza na ya pili ya Katiba kwa kuwa ni maoni yanayotoka kwa Watanzania.
Kwa mujibu wa tamko hilo ambalo chanza imeona nakala yake, tume hiyo imeelezea matumaini na furaha ya Watanzania kwa ujio wa Rasimu ya pili Katiba iliyosheheni utu na misingi ya kujali maslahi ya wote.
Tamko hilo lililosainiwa na Mwenyekiti wa tume hiyo, Askofu Mkuu Paulo Ruzoka, limetokana na mkutano wa kitaifa wa wajumbe wa Kamati za Majimbo za Haki na Amani wa kanisa hilo na CPT, waliokutana kwenye kituo cha Kiroho cha Mbagala jijini Dar es Salaam, Februari 5 na 6 mwaka huu.
Limeeleza kuwa walikutana kutafakari juu ya mchakato wa kuandika Katiba mpya na wajibu wa Kanisa Katoliki katika utume wake wa kinabii wa kulinda na kujenga haki na amani ya nchi kama Rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Tamko hilo limetoa mapendekezo baada ya kuipitia Rasimu hiyo kwa kuongozwa na uchambuzi makini uliowasilishwa na Sekretarieti ya Tume ya Kanisa hilo kuwa suala la la muundo wa Muungano wa serikali tatu siyo jambo kuu kuliko mengine yote katika Rasimu.
“Muundo wa serikali mbili haukutatua matatizo ya msingi bali ulilimbikiza kero zilizosababisha Zanzibar kujiundia Katiba yake mpya ya mwaka 2010 bila kushauriana na Tanzania Bara (Tanganyika),” imesema sehemu ya tamko hilo.
Aidha, Tume hiyo ilisema pendekezo la serikali tatu lililowekewa mazingira tekelezi yakitoa mwanya wa kuboresha muundo huo kwa njia wazi, shirikishi na za kidemokrasia lina tija kubwa ya kuturudishia hali ya kuwa wamoja.
Tamko hilo limefafanua kuwa mihimili mikuu mitatu ya serikali ni taasisi mpya kwa mujibu wa rasimu ya pili zitakazoongoza, kuratibu na kuwajibisha kila kiungo cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zikiwamo serikali za nchi washirika.
Wataalamu hao wamesema Rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni ya watu na siyo ya wanasiasa au vyama vya siasa wala asasi za kidini na imewataka Watanzania kufurahia kupatika kwa Rasimu hiyo itakayokuwa nguzo ya umoja wa nchi katika Katiba.
“Katiba yetu lazima isiruhusu wachache wenye nguvu za kisiasa, kiuchumi na kiutawala kutumia vibaya uwezo wao na kusababisha utengano kitabaka katika jamii huku wakijinufaisha kwa kutumia rasilimali za nchi zilizo za wote,” limesema tamko hilo.
Aidha, Tec imesema haki ya mtu ya kuishi lazima ilindwe na Katiba kuanzia pale mimba ya binadamu inapotungwa kwa mama na katika hatua zake zote za kumhudumia mama mjamzito.
Tume hiyo imeridhia pawepo na udhibiti thabiti wa mienendo ya namna hiyo na uwajibishaji makini kwa wabadhirifu wa mali ya umma na kwamba Katiba ni chombo hai kwa ajili ya kuhudumia jamii na siyo jamii kuhudumia Katiba.
Imesema kwa sababu hiyo yapaswa kuthubutu kubuni njia mbadala ili kukuza kipato cha raia wa kawaida na kuboresha huduma za jamii kwa kuwa na mipango endelevu ya kiuchumi.
“Kumtambua Mungu na kumtaja katika Katiba kuna maanisha kukiri kwetu uwapo wake aliye Muumba wetu na vitu vyote katika kuheshimiana kiutu, ni chimbuko la utu wa binadamu, kwa kuwa katika Wimbo wa Taifa tunamwomba Mungu baraka zake ili tufanikiwe na tuishi kwa amani, ni hekima na busara kumkiri katika sheria mama ambayo ni Katiba,” limesema.
Tec imesema kwa kipindi cha Bunge Maalum la Katiba wanataka mambo ya msingi kutambuliwa ambayo ni Watanganyika na Wazanzibar kuwa na nia madhubuti ya kuwa wamoja.
“Ulimwenguni hakuna katiba yoyote kamilifu, yatupasa tuanze na rasimu iliyopendekezwa na tuendelee kuiboresha pale itakapobidi…tunawasihi wajumbe wa Bunge kuweka kando itikadi zao kama walivyofanya wanatume ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika Rasimu ya pili,” lilisema tamko hilo.
Baraza hilo limesema haki za binadamu za kisiasa, kiuchumi na kijamii zipatikane na kufurahiwa na wote, umaskini na ufinyu wa bajeti ya serikali ni visingizio vya mamlaka kutokutoa haki kwa wote.
Aidha, Tec imewataka Watanzania kwa dhamira moja kuliombea na kulisaidia Bunge Maalum la Katiba, liweze kufanya kazi yake kwa ustadi na kujali maslahi ya Taifa na wananchi wote wa Tanzania.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment