Sio kawaida yangu kuanza somo na ushuhuda ila hili nimeamua kulianza na ushuhuda kutokana na unyeti wa somo lenyewe.
Miaka kadhaa iliyopita kuna dada mmoja ambaye nilikuwa namfahamu, 
alikuwa akiteswa sana na hali ya kutopata watoto. Ni jambo lilikuwa 
linamsumubua sana kwenye ndoa yake na alikuwa amenishirikisha na 
nikamwandalia kitini chenye ahadi za Mungu juu ya kupata watoto na 
nikamhakikishia kuwa ahadi za Mungu zote katika Kristo Yesu ni ndiyo na 
amina. 
Lakini pamoja na hayo bado huyu dada akaendelea kuteswa na hiyo hali ya 
kutopata watoto. Ikitokea anapata uja uzito ule uja uzito unatoka ukiwa 
na miezi michache sana. Hii ilinisumbua sana kama Mchungaji wake maana 
neno la Mungu lipo wazi kuwa hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba wala 
aliye tasa miongoni mwa watu wa Mungu. Neno la Mungu lipo wazi kabisa 
kuwa watoto ni Baraka itokayo kwa Mungu na uzao wa tumbo ni thawabu 
Yake. Hii ilinisumbua sana maana huyu dada alikuwa ameokoka na hapakuwa 
na sababu yoyote ya msingi kwanini awe anateswa kwa namna hii.
Siku moja nikiwa naliwaza hili ili nipate solution ya Kimungu juu ya 
tatizo la huyu dada nikasikia moyoni maneno yanayopatikana kwenye moja 
ya maandiko nitakayotumia katika fundisho hili: “Agano na mauti, 
mapatano na kuzimu.” Nilishtuka sana maana niliisikia as clear as wewe 
unavyoweza kusikia mimi nikisema na wewe. Nikauliza huko huko moyoni, 
Lakini Mungu huyu ni mtoto wako ana agano na wewe na mapatano na wewe 
kupitia damu ya Yesu, iweje tena awe na agano na mauti na mapatano na 
kuzimu? Nikasikia tena maneno hayo hayo yakijirudia. Nikajua this is 
serious. Nikauliza tena huko moyoni How? Nikasikia wazi wazi “BLOOD 
GUILTINESS.” Nikashtuka maana nilielewa sasa Mungu anasema nini. 
Nikauliza Mungu huyu binti kaua mtu? Jibu lilinishtusha sana. Aliniambia
 ameua watu sio mtu. Nikasema kwa sauti nikiwa peke yangu, “My God! 
Whaaaaaaaat?!!!!!!” akarudia tena, ameua watu sio mtu. Sasa hapo naongea
 kwa sauti ya wazi wakati Yeye Mungu ananisemesha moyoni. 
Nilikaa sakafuni chumbani kwangu nikasema, Mungu hapa sikuelewiiiii! 
Kaua watu gani! Akaniuliza hivi wewe hujui watu wanavyo ua na hawajioni 
kuwa ni shida? Nikamdaka hapo hapo. Nikaambiwa mwite muulize. 
Nilimtafuta huyu binti nikamwambia nahitaji kuonana na wewe. Tukapanga 
siku atakayokuja kuniona alipokuja sikumzunguka nikamwuliza binti embu 
niambie umemwua nani na umewaua wangapi maana Mungu ananiambia hupati 
watoto kwa kuwa wewe ni mwuaji. Alishika kichwa akasema “My God!!!” 
akainama huku machozi yanamtoka. Nikamwuliza binti umeshawahi kutoa 
mimba? Akaniambia ndiyo mchungaji. Sikutaka kumpotezea wakati maana 
alihitaji suluhisho la haraka kwa ajili ya uteka wake. Nikamwambia sasa 
mwanangu kutoa kwako mimba kumegeuza tumbo lako la uzazi badala ya kuwa 
chanzo cha uhai na mahali pa salama pa kumkuza mtoto, pamekuwa kiwanda 
cha kuulia watoto wanaoingia hapo. Tumbo lako lina agano na mauti na 
mapatano na kuzimu kwa sababu umekuwa ukiua watoto ambao wamekuwa 
wakiingia humo ndani. Akaniambia ni kweli Pastor. Nikamwambia unateswa 
na hatia ya damu na hilo litabidi tu livunjwe. Neno linasema tuungamiane
 dhambi zetu sisi kwa sisi na kuombeana tupate kupona. Hapo akawa 
kaungama dhambi yake. Nikamwongoza sala ya kuvunja hilo agano na mauti 
na mapatano na kuzimu sawasawa na ilivyofunuliwa kwenye neno. Nikaomba 
naye akalia sana. Akasema sasa Pastor nina amani. Nikamwambia nenda sasa
 kazae. Namshukuru Mungu ule uteka wa miaka ulivunjwa na sasa huyu dada 
na mumewe wana watoto. 
Kama umeua kwa kukusudia au kutokukusudia inawezekana unateswa na shida 
hii ya hatia ya damu. Inawezekana kabisa umeingia katika agano na mauti 
na mapatano na kuzimu ambayo yanakutesa na kuzuia au kuua vitu vyako 
vingi.Tutalifuatilia hili jambo kimaandiko na kuleta suluhisho la 
msalaba kwa tatizo hili gumu ambalo linatesa maisha ya wengi.
Daudi alifanya kosa la kuzini na mke wa mtu akampa huyo mke wa mtu mimba
 alafu akafunika hilo kosa kwa kuua mumewe. Kama ambavyo sisi tunafanya 
uasherati au uzinzi tunampa mtu au kupewa mimba na katika jitihada za 
kufunika hiyo aibu tunaamua kuitoa hiyo mimba ambayo kimsingi ni kuua. 
Yai la mwanamke likishakutana na mbegu ya kiume na mimba ikatungwa Yule 
ni mtu katika hatua zake za awali. Hutoi bonge la damu au bonge la nyama
 unaua mtu na unamwaga damu usiyo na hatia. 
Daudi alipogundulika alilikwenda mbele za Mungu kwa toba lakini pamoja na toba akaomba aponywe na damu za watu. 
Zaburi 51: 14.
14Ee MUNGU, Mungu wa wokovu wangu,Uniponye na damu za watu,Na ulimi wangu utaiimba haki yako.
Damu za watu zilileta shida katika maisha ya Daudi.
Naipenda inavyosema kwenye bibilia ya kiingereza:
“Deliver me from the guilt of bloodshed,……”
Kimsingi anaomba akombolewe na hatia ya damu aliyoimwaga.
Utashangaa pale awali Daudi alipotubu baada ya nabii Nathan kuja na 
kuiweka wazi dhambi yake, aliambiwa amesamehewa ila athari za dhambi 
yake hii ziliachiliwa juu yake na ndicho Daudi alichokuwa anashughulikia
 hapa kwenye haya maombi ya Zaburi 51.
I Samweli 12: 10 – 14.
10Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, 
ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako. 11BWANA asema hivi, Angalia, 
nitakuondokeshea uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako 
mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako 
mbele ya jua hili. 12Maana wewe ulifanya jambo lile kwa siri; bali mimi 
nitalifanya jambo hili mbele ya Israeli wote na mbele ya jua. 13Daudi 
akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi. Nathani akamwambia Daudi, 
BWANA naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa. 14Lakini, kwa kuwa kwa tendo
 hili umewapa adui za BWANA nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto 
atakayezaliwa kwako hakika yake atakufa.
Pamoja na kwamba alisamehewa dhambi yake lakini kuna mauti ilifunguliwa 
kuingia kweye nyumba ya Daudi kupitia kitendo chake cha kuua mtu. 
Unapotoa mimba unaifungulia mauti kuingia katika maisha yako hususa 
kwenye uzazi wako. Haijalishi ni mwanaume au ni mwanamke. Ukitoa mimba 
au kusaidia kutoa mimba umeua au umesaidia kuua.Daudi alitamani 
kumjengea Mungu nyumba lakini akaambiwa hataweza kujenga kwa sababu 
mikono yake ilikuwa na damu. Hii roho ya mauti na kuzimu unayoifungulia 
maishani mwako kwa njia ya kuua itakugharimu sana. Itakunyanganya mpaka 
uwezo wa kujenga. 
Bahati mbaya sana sio wasioamini tu wanatoa mimba siku hizi mpaka 
waaminio na mbaya zaidi waliyo ndani ya ndoa. Aibu ya mama kushika mimba
 mapema mno baada ya mtoto kuzaliwa labda miezi michache inawafanya 
waitoe. Ni kuua huko. Ni kuuondoa uhai wa mtu asiye na hatia. Umemnyima 
mtu asiuone mwanga wa jua, yote kwa sababu ya kuficha kitu. 
Mungu anachukia mikono iliyo myepesi kumwaga damu.
Mithali 6: 16, 17.
16Kuna vitu sita anavyovichukia BWANA;Naam, viko saba vilivyo chukizo 
kwake.17 Macho ya kiburi, ulimi wa uongo,Na mikono imwagayo damu isiyo 
na hatia;
Kama Mungu anaichukia mikono imwagayo damu niambie ni kwa namna gani 
mikono hiyo hiyo kazi zake zinabarikiwa? Unakwama kimaisha, kitaaluma, 
kibiashara, kikazi, kimasomo, yote kwa dhambi ya kumwaga damu isiyo na 
hatia. Mbaya zaidi kuna kuwa na mauti imeachiliwa inayoharibu hata 
kilichopo.
Kaini aliimwaga damu ya nduguye Habili ikamletea madhara makubwa sana.
Mwanzo 4: 8 – 12.
8Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]. Ikawa walipokuwapo 
uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye, akamwua. 9BWANA akamwambia 
Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa 
ndugu yangu? 10Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako 
inanililia kutoka katika ardhi. 11Basi sasa, umelaaniwa wewe katika 
ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono 
wako; 12utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu 
asiye na kikao duniani.
Kaini alikuwa ni mkulima na aliitegemea ardhi na bado hakuzingatia hilo,
 akaimwaga damu ya nduguye kwenye uwanda ule ule ambao alikuwa 
anautegemea umpe mazao. Ile damu ikamlilia Mungu. Alinyamazisha sauti ya
 Habili lakini hakunyamazisha sauti ya damu ya Habili. Mungu akamwambia 
Kaini kuwa amelaaniwa katika ardhi iliyopokea damu ya ndugu yake, 
atakapoilima haitampa mazao na sio hivyo tu atakuwa mtoro au mzururaji 
na mtu asiye na makao. Ninaamini huu uzururaji wa Kaini na kutanga tanga
 kwa Kaini kulisababishwa na yeye kudhani ni hapo alipo ndo pana shida 
so anajaribu na kwingine na kwingine na kwingine asijue uhusiano wake na
 ardhi ambao ndo chanzo cha mapato yake umeharibiwa kupitia tendo lake 
hilo la kumwaga damu. Kaua ili yeye hakuuawa bali shughuli zake ndo 
zikauawa. 
Unatumia kipato chako kuua alafu bado unategemea utaendelea tu 
kubarikiwa kupitia chanzo hicho. Ndo ushaachilia mauti kwenye shughuli 
zako. Umefanikiwa kuficha aibu ila hujafaikiwa kuzuia athari za uuaji 
wako.
Musa aliua mtu akamzika akijua hakuna aliyemgundua, kumbe kuna 
aliyemwona. Sawa umewaficha watu, je shetani umemficha, Mungu naye 
umemficha? Itakuja kutakwa tu mikononi mwako. Umeinyamazisha sauti ya 
kimwili ila ya kiroho umeshindwa kuinyamazisha na ndo inayolia kisasi 
kisasi kisasi. Hakuwa na hatia na ukamwua. Huwezi kuepuka athari za 
mauti na kuzimu.Musa akaja kujua watu wamejua na hiyo ikaifungulia hatia
 ya damu maishani mwake akakimbia na kutokomea jangwani kwa miaka 40 na 
kuchelewesha ukombozi wa wana wa Israeli kwa miaka 30. 
Maana Mungu alimwambia Ibrahimu kuwa wana wa Israeli watakaa utumwani 
miaka 400 lakini wakaishia kukaa utumwani miaka 430 kwa sababu ya hatia 
ya damu iliyomkamata Musa. Alijaribu kufanya miaka kumi kabla ya wakati 
akaachilia hatia ya damu ambayo ilimkimbiza kwa miaka 40. Usiendelee 
kuiacha hatia ya damu ikutese. Inakucheleweshea mambo yako bila sababu. 
Yesu ameshakufa msalabani amechukua dhambi zako mpaka hatia yako ya 
damu. Damu Yake iliyomwagika kwa ajili yako inakunenea mema kuliko damu 
ya kina Habili au hao ambao umemwaga damu zao pasipo hatia yoyote.
Nilishangaa sana nilipokuwa nafuatilia kazi za damu ya Yesu. 
Ina samehe na kukomboa.
Efeso 1: 7.
7Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.
Utasamehewa na kukombolewa na athari mbaya za hatia ya damu kama ukitubia makosa yako ya kuua na kumwaga damu isiyo na hatia. 
Kuna wakati Daudi alipokuwa mfalme kulikuwa na ukame katika ufalme wake 
miaka mitatu mfululizo. Alipomwuliza Bwana akakuta ni hatia ya damu ndo 
sababu ya hayo majanga.
II Samwli 21: 1.
1 Kulikuwa na njaa siku za Daudi muda wa miaka mitatu, mwaka kwa mwaka; 
naye Daudi akautafuta uso wa BWANA. BWANA akasema, Ni kwa ajili ya 
Sauli, na kwa nyumba yake yenye damu, kwa kuwa aliwaua hao Wagibeoni.
Ukame ule ulisababishwa na kiti cha Ufalme na ikafungulia shida kwenye 
himaya nzima iliyo chini ya kiti hicho Ukame. Wewe nawe ni mfalme wa 
Kahimaya kako. Damu isiyo na hatia uliyo mwaga au kwa kutoa mimba au 
vinginevyo imesababisha huo ukame unaopitia katika maeneo mbali mbali ya
 maisha yako. Daudi akataka kujua nini kifanyike na jawabu likawa watu 
wa nyumba ya mhusika wa kuua wauawe ili kuridhisha kisasi cha damu 
iliyomwagika na ilipofanyika hivyo, mvua ikanyesha. Sisemi lazima mtu 
afe. Kuna aliyekufa ili kuvunja hatia ya damu inayokutesa na Jina Lake 
ni Yesu maana imeadikwa adhabu ya amani yetu iliwekwa juu Yake. 
Unapokuja kwa Yesu na kuikiri dhambi yako ya kuua utapokea msamaha na 
athari za hiyo dhambi na hatia ya umwagaji damu itavunjwa maishani mwako
 kwa Jina la Yesu na mvua itaanza kunyesha tena. Ukame utavunjwa na 
utaanza kuexperience uhuru kamili katika uchumi wako. Fikiria taifa zima
 liliingia kwenye maafa ya kiuchumi kwa sabau ya hatia ya damu.
Je kuna uwezekano kuna maafa ya kifedha maishani mwako kwa sababu ya 
hati ya damu? Je kuna vurugu za kifamilia kwako kwa sababu ya hatia ya 
damu? Je inawezekana mambo yako hayaendi kwa sababu ya hati ya damu?
Ndugu tengeneza ukitumia mwanga unaopata kwenye hili somo ufunguliwe 
utembee katika uhuru ambao Kristo amekununulia kwa uhai na damu Yake.
Wakati wa Agano la Kale kulikuwa na kitu kinaitwa miji ya makimbilio.
Kumbukumbu 19: 1 – 6.
1 BWANA, Mungu wako, atakapoyakatilia mbali hayo mataifa yenye nchi 
akupayo BWANA, Mungu wako, nawe ukawafuata, na kukaa katika miji yao, na
 katika nyumba zao; 2itenge miji mitatu iwe kwako katikati ya nchi yako,
 akupayo BWANA, Mungu wako, kuimiliki. 3Itengeze njia, igawanye na 
mipaka ya nchi yako, akurithishayo BWANA, Mungu wako, iwe mafungu 
matatu, ili kwamba kila mwenye kuua mtu apate kukimbilia huko. 4Na hii 
ndiyo hukumu ya mwenye kuua mtu, atakayekimbilia huko awe hai; 
atakayemwua mwenziwe pasipo kukusudia, wala hakumchukia tangu hapo; 
5kama aingiapo mtu na mwenziwe mwituni kwenda kukata kuni, akapeleka 
mkono wake na shoka ili kukata mti, likatoka shoka katika mpini, 
likampiga yule mwenziwe hata akafa; basi na akimbilie katika miji hii 
mmojawapo awe hai; 6asije akaandamiwa mwuaji na mwenye kulipiza kisasi 
cha damu, moyo wake ukali na hasira, akampata kwa njia kuwa ndefu, 
akamwua; wala hana haki ya kuuawa, kwa kuwa hakumchukia tangu hapo.
Hii miji ya makimbilio ilikuwa kwasababu ya wale ambao wameua bila ya 
kukusudia ili wakimbilie huko ili mlipiza kisasi cha damu asije akawaua 
wakati ni jambo wamelifanya kwa kutokukusudia. Hii ina maana kuwa kama 
mtu alifanya kwa kukusudia asingeweza kukimbilia kwenye hii miji. Hata 
angekimbilia mlipiza kisasi cha damu angekuja tu kudai atolewe. Sasa 
wewe umeua kabisa kwa kukusudia alafu unajifanya unakimbilia kwa Yesu 
kujificha. Hutaepuka kisasi cha mlipiza kisasi cha damu isipokuwa Yesu 
kaingilia kati na kwa njia ya wewe kuitubu hiyo dhambi maususi, ili 
sadaka ya Yesu ya Uhai na Damu Yake vichukue nafasi yako wewe ili 
kukuepusha na athari za mlipa kisasi cha damu.Usifanye shingo yako 
ngumu. Usipotezee maana haipotezeki. Mruhusu Yesu akuweke huru na athari
 za mlipa kisasi cha damu uliyomwaga ili wewe uwe huru. 
Unapomwaga damu ili kuficha majanga yako, umekimbilia chini ya maneno 
yasiyo ya kweli na kwa njia hiyo umeachilia agano la mauti na mapatano 
ya kuzimu. Ni hilo agano na mauti na hayo mapatano na kuzimu ndo yanaua 
kazi zako, furaha yako, amani yako, na vitu vingine vilivyokuuzunguka.
Isaya 28: 15.
15Kwa sababu mmesema, Tumefanya agano na mauti, tumepatana na kuzimu; 
pigo lifurikalo litakapopita, halitatufikia sisi; kwa maana tumefanya 
maneno ya uongo kuwa kimbilio letu, tumejificha chini ya maneno yasiyo 
kweli;
Ukifanya tu maneno ya uwongo kuwa kimbilio na kujificha chini ya maneno 
yasiyo kweli unajiingiza kwenye agano na mauti na mapatano na kuzimu.
Umeificha hiyo mimba kwa kuua, umeunyamazisha huo ukweli kwa kuua, haya sasa mauti ina wewe, kuzimu haikuachi.
Ila kuna habari njema hapa:
Isaya 28: 16.
16kwa ajili ya hayo Bwana, MUNGU, asema hivi, Tazama, naweka jiwe katika
 Sayuni, liwe msingi, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni lenye 
thamani, msingi ulio imara; yeye aaminiye hatafanya haraka.
Jiwe hili lililowekwa Sayuni ni Yesu Kristo na amewekwa mahususi 
kushughulika na hili agano na mauti, na haya mapatano na kuzimu.
Isaya 28: 18.
18Na agano lenu mliloagana na mauti litabatilika, tena mapatano yenu 
mliyopatana na kuzimu hayatasimama; pigo lifurikalo litakapopita, ndipo 
ninyi mtakapokanyagwa nalo.
Njoo kwa Yesu ubatilishiwe hilo agano na mauti na kuangushiwa chini hayo mapatano na kuzimu.
Mwendee Yesu na mwanga huu uliyoupata na ufunguliwe kabisa na athari 
mbaya za Hatia ya damu kwa Jina la Yesu. Usisahau kuvunja hilo agano na 
mauti na mapatano na kuzimu kwa Jina la Yesu ili uwe huru.
UMEBARIKIWA NA UMEREHEMIWA.

No comments:
Post a Comment