.

.

.

.

Friday

Yajue Mambo Yanayowatofautisha Wanaofanikiwa na Wanaofeli Maishani



Ukitaja Harry Porter watu wengi wanajua kuhusu Movies na Vitabu maarufu sana vilivyoandikwa na Mwandishi maarufu wa uingereza J.K Rowling ambaye amefanikiwa sana kupitia kazi zake za uandishi.Lakini kitu ambacho watu wengi hawajui kuhusu J.K Rowlings ni mambo aliyoyapitia katika maisha yake hadi kufika hapo alipo sasa hivi.
Mwaka 1990 ndio kwa mara ya kwanza alipata wazo la kuandika kuhusu Harry Porter na wazo hili lilikamilika zaidi alipokuwa safarini kwenye treni akitokea Manchester kwenda London.Mara baada ya kuona ni wazo linaloweza kubadilisha maisha yake aliamua kulifanyia kazi kwa haraka na akaanza kuandika kwa bidii sana.Hata hivyo,mwaka huohuo mama yake alifariki baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Miaka miwili baadaye alihamia ureno ambako alianza kuwa mwalimu wa lugha ya kiingereza ambako pia alikutana na mwanaume ambaye alimuoa na alipata mtoto wa kike.Mwaka mmoja baadaye (1993) aliachwa na akaamua kurudi uingereza kwenye mji wa Edinburg wakati huo alikuwa tayari ameandika sura 3 za kitabu chake cha Harry Porter.Aliporudi Uingereza maisha yalikuwa magumu saidi na alijiona kama vile ndoto yake ya kuandika kitabu imeshakufa kwani alikuwa hana kazi,ameachwa na ana mtoto wa kumtunza.Ghafla akajikuta yuko kwenye msongo  mkubwa wa mawazo(stress) na mfadhaiko(depression) mkubwa sana.Hivyo aliamua kujiorodhesha katika mpango wa serikali  ambao unasaidia watu maskini(Government welfare program).
Mwaka 1995 alijaribu kupeleka kitabu chake kwa wachapishaji zaidi ya 12 na wote walikataa kuchapisha kitabu chake lakini mwaka mmoja baadaye kampuni moja ndogo(Bloomsbury) sana ikakubali na kumchapishia kopi 1000 tu na huku 500 zikigawiwa kwenye maktaba na alilipwa paundi 1500 za utangulizi.Miaka miwili baadae(1997 na 1998) kitabu chake kikashinda tuzo toka Nestle Smarties na British Book Award kama kitabu bora cha watoto cha mwaka.Baada ya hapo Rowling ameuza zaidi ya kopi milioni 400 ya kitabu chake na ndio anachukuliwa kama mwandishi mwenye mafanikio zaidi nchini Uingereza.
Jambo kubwa la kulijua hapa ni kuwa bila kujali una ndoto ya kufanya nini ama unataka kukamilisha jambo gani katika maisha yako ni lazima utapitia nyakati ngumu na zenye kukatisha tamaa katika maisha yako.Kuna watu wengi sana ambao wameshindwa kufanikiwa katika maisha yao sio kwa sababu hawana uwezo ama kipaji cha kuwafanya wafanikiwe lakini kwa sababu wameshindwa kuendelea mbele katika kufuatilia malengo yao hasa baada ya kushindwa mara kadhaa baada ya kujaribu.Kama kweli unataka kufanikiwa kwa kiwango cha juu sana lazima uwe mtu ambaye hauko tayari kushindwa katika jambo lolote lile kwenye maisha yako.
Kuna watu wengi sana wanaokufa na vipaji vyao,wanakufa na uwezo wao ambao ungeweza kuwasaidia sana kubadilisha maisha yao.Nawe najua unasoma Makala hii kwa sababu unatamani kufanikiwa kufikia kilele cha ndoto yako,lakini ukweli ni kuwa kama hautakuwa tayari kuchukua hatua madhubuti basi itakuwa ngumu sana kwako kufanikiwa.Mafanikio huanza na uamuzi thabiti unaotoka ndani ya moyo wako kuwa kweli unataka kupiga hatua katika maisha yako.Uamuzi huu hakuna mtu anayeweza kukufanyia isipokuwa wewe mwenyewe,ni lazima ufike sehemu uufanye.
Mara nyingi uamuzi wa namna hii unaweza kutokana na kutaka kuepuka maumivu(To avoid pain) au kutokana na kutamani kupata raha (to seek pleasure).Historia za wengi waliofanikiwa ni lazima walihusisha kitu kimojawapo kati ya viwili.kuna watu ambao walipitia wakati mgumu sana katika maisha yao na kwa sababu hiyo walijikuta wamefika sehemu wamechukia maisha ya umaskini na wakakata shauri ndani ya mioyo yao la kutaka kuanza safari mpya ya mafanikio,kwa maneno mengine hawataki kabisa aidha wao au ndugu ama watoto wao wapitie hali ya mateso ambayo wao wamepitia.Kwa upande mwingine kuna watu ambao waliishi maisha ya kawaida tu lakini wameona jinsi wengine ambavyo wamefanikiwa katika maisha yao na  wao wametamani kuishi kama hao wengine.Katika maisha hakuna mtu anayefanikiwa kwa bahati mbaya,hata wewe kama kweli unataka kufanikiwa ni lazima uamue kuanzia leo.
Swali la msingi ambalo ni muhimu kujiuliza ni kuwa;hivi kwa nini watu wengi hawafanikiwa katika maisha na wachache ndio huwa wanafanikiwa?Ziko sababu kuu 4 ambazo zinawafanya watu washindwe kufanikiwa katika maisha yao:
• HOFU YA KUFANYA JAMBO JIPYA
Tafiti za kisaikolojia zinaonyesha kuwa kila mtu huwa hapendi kuondolewa kutoka mahali alipopazoea(comfort zone).Hii ndio maana kuna watu kanisani kila jumapili watakaa upande huohuo na wengine kiti kilekile na wakikuta kuna mtu amekaa huwa wanaona kama vile wamekalia kiti chao.Hata nyumbani ukichunguza vizuri kuna watu huwa wanakaa kochi hilohilo ama kiti hichohicho wakati wa kula hata kama hajawahi kupangiwa kuwa akae hapo.Ndivyo ilivyo katika maisha ya kawaida watu wengi huwa hawapendi kubadilika.Kuna watu kila wakienda na kurudi kazini wanapita njia ileile kwa miaka nenda rudi,hata kama kuna njia nyingine hawajawahi kujaribu kabisa.
Hebu jichunguze kitu ambacho unakifanya kwa sasa hivi umekuwa ukikifanya kwa muda gani na kwa nini haujabadilisha hadi leo.Leo fikiria kuna kitu gani kipya ambacho unaweza kuanza kukifanya kwenye maisha yako?Usikubali mwaka huu uiishe kabla haujaanza kufanya kitu kipya tofuati na unachofanya sasa hivi.Kumbuka kuwa Henry Ford alisema ““If you always do what you’ve always done, you’ll always get what you’ve always got.”(Ukiendelea kufanya mambo yaleyale ambayo umekuwa ukifanya sikuzote basi utapata matokeo yaleyale ambayo umekuwa ukiyapata)
• HOFU YA KUFELI/KUSHINDWA
Sababu nyingine inayowafanya watu washindwe kufanikiwa ni ile hofu ya kushindwa.Kuna watu wengi sana ambao wameogopa kufanya jambo fulani kwenye maisha kwa sababu ya hofu ya kuwa watashindwa.Mara nyingi,wazo la kwanza ambalo watu huwajia katika akili yao inapofika kufanya jambo fulani huwa ni “itakuwaje nisipofanikiwa”.Kuna watu wanaogopa kufanya biashara kwa sababu ya kuwa na hofu ya kupata hasara,kuna watu wanaogopa kuomba kazi mahali kwa sababu ya hofu ya kukataliwa,kuna watu wanaogopa kuanza kulima kwa sababu ya hofu ya kupata hasara. Mtu mmoja mwenye hekima alisema  — “Everything you want is on the other side of fear”(Kila kitu ambacho kwa sasa hauna na unakitaka,kipo upande wa pili ukishaivuka hofu).Mafanikio yako yamejificha nyuma ya hofu inayokukabili.
Kama kweli unataka kufanikiwa katika maisha yako ni lazima uanze kuishi katika namna ambayo hofu ya kufeli haina nafasi.hebu jiulize leo,kuna mambo mangapi ambayo unatamani kuyafanya lakini kinachokuzuia ni hofu ya kushindwa?Leo anza kuishinda hofu hiyo na anza kuchukua hatua mara moja.Kuanzia leo ningekushauri kutumia kanuni hii aliyowahi kuisema Jack Carnfield aliposema –‘'Don't worry about failures, worry about the chances you miss when you don’t even try”(Usiogope kufeli bali ogopa mafanikio ambayo unaweza kuyakosa uanpoogopa kujaribu).
• KUTUMIA VISINGIZIO VYA KUTOKUWEZEKANA
Jambo la tatu linalosababisha watu wafeli katika maisha yao ni ile hali ya kutumia visingizio walivyonavyo katika maisha yao.Wengine watatumia visingizio vya kutokusoma/kutokuwa na elimu ya kutosha,wengine watatoa visingizio vya hali mbaya ya uchumi,wengine watatoa visingizio vya familia walizotoka n.k./UKweli ni kuwa wakatai wowote ule ukitaka kupata visingizio vya kutofanya jambo fulani basi utavipata vingi sana,ila kama kweli unataka kufanikiwa ni lazima uamue kutokuwa mtu wa visingizio kabisa katika maisha yako. Jim Rohn  aliwahi kusema  'If you really want to do something, you'll find a way. If you don't, you'll find an excuse”(Kama kweli uantaka utatafuta namna ya kupata,ila kama hautaki basi utatafuta visingizio)
Kuna mambo mengi leo ukiulizwa kwa nini huyafanyi utajikuta unatoa visingizio,kumbuka kuwa kila unapotoa visingizio basi unapoteza uwezo wako wa kutatua changamoto inayokukabili.Kuanzia leo amua kuwa mtu ambaye hautoi visingizio na badala yake uwe mtu wa kuchukua hatua.Watu wanaotoa visingizio kila siku watamlaumu mzazi,ndugu ama rafiki.Amua kuachana na visingizio kuanzia leo-Anza hivyo biashara,anza kilimo,chukua hatua.
• KUJILINGANISHA NA WENGINE
Jambo la nne linalowasababisha watu wafeli kabisa ni ile hali ya kujilinganisha na wengine.Ni vyema nianze kwa kukuambia kuwa wewe umeumbwa kuwa wa tofauti,hakuna mtu yoyote yule ambaye unafanana naye kabisa.Mungu alipokuumba aliweka ndani yakio uwezo wa kipekee na uwezo wenye nguvu sana wa kubadilisha maisha yako kabisa.Usifanye kosa hata siku moja kujilinganisha na wengine.Kuna watu wengi sana waliumbwa na uwezo mkubwa kama tembo ila kwa sababu wamekuwa wakiishi na watu wenye uwezo mdogo kama sungura wamejikuta wanaishi maisha ya kawaida sana.
Hata kama kila mtu anaishi maishi ya kawaida,ya chini,ya kushindwa-Kumbuka wewe haujauumbwa uishi hivyo.Wewe umeumbwa kuwa mshindi,wewe umeumbwa kufanikiwa,wewe umeumbwa kuinuka hadi juu.Usiangalie wengine wanaoishi kawaida nawe ukajiweka kuwa mmoja wao,usiangalie kiwango cha maisha cha familia yako,usiangalie kiwango cha maisha cha majirani na ndugu zako-HAPANA.Wewe nafasi yako sio hapo,wewe nafasi yako ni juu zaidi.Inawezekana leo unaishi maisha ya taabu na yenye kukatisha tamaa,unachotakiwa kujua ni kuwa hayo ni maisha ya mpito na unaweza kuyabadilisha kama ukiamua.
Kama kweli umesshafanya maamuzi ya kuamua kufanikiwa katika maisha yakobasi ni vyema ukajua namna ya kuanza kuishi kuanzia leo ili uanze safari yako ya mafanikio.Ziko njia tatu unazoweza kuanza kuzitumia kuanzia leo ili ujiunge na wale ambao wanafanikiwa kila siku:
• AMINI KWAMBA INAWEZEKANA.
Jambo la kwanza kabisa katika safari yako ya mafanikio ni uwezo wako wa kuamini kuwa unalotaka kufanikiwa linawezekana.Watu wengi sana huwa wanafeli hata kabla hawajajaribu kwa sababu kabla hawajaanza,utasikia-“Hili haliwezekani”.Kama kweli unataka kufanikiwa ni lazima uwe na imani kuwa inawezekana;ndio-Inawezekana kuwa tajiri,inawezekana kupona,inawezekana kufaulu mitihani,inawezekana kuanzisha biashara n.k
Mara nyingi hatua hii huwa ni ngumu sana kwa muda mrefu tunakuwa tumeaminishwa kuwa kile tunachokitaka hakiwezekani.Imani hizi hutokana na maneno tuliyoambiwa na wazazi wetu,walimu wetu,marafiki ama mazingira ambayo tumekulia.Kutokuwezekana kwa jambo mara nyingi ni fikra ambayo imejengeka ndani kabisa ya ubongo wetu na hakuna namna tunaweza kuitoa bila kuamua na kutumia mikakati madhubuti.
Ili fikra ya kutokuwezekana iondoke kabisa katika akili yetu tutahitaji kujiambia wenyewe mara nyingi zaidi kuwa inawezekana kuliko mara ambazo tumeshawahi kusikia kuwa haiwezekani.Hii ndio maana kuna wakati utatakiwa kuchukua malengo yako na ukae peke yako mahali na uyasome na useme kwa sauti-“Haya yote yanawezekana”.Kila wakati wazo la kuwa utafeli,utapata hasara au wazo la haiwezekani linapokuja ndani yako basi jiambie kwa sauti kuwa inawezekana.
Je,kuna jambo lolote ambalo ulikuwa unalitamani kulifanya ila unakwa unaona kama vile halitawezekana?.Leo lichukue jambo na useme-Hili nalo linawezekana.
• PATA MAARIFA UNAYOHITAJI
Ili uweze kufanikiwa katika malengo yako ni lazima ujijenge katika maarifa muhimu yanayotakiwa kukusaidia kutimiza malengo yako.Kama unataka kufanya biashara basi hakikisha kuwa unapata ujuzi wa kutosha kuhusiana na biashara unayotaka kufanya.Uwe mtu ambaye uko tayari kila wakati kugharamia maarifa ambayo yanaweza kuwa msaada kwako katika kutimiza malengo yako.
Uwe tayari kutumia pesa yako kwa ajili ya kununua vitabu,CDs,DVDs n.k ili kujenga uwezo wako wa kufuatilia na kutimiza malengo yako.Hakikisha kuwa kila siku haipiti bila kujifunza kitu kipya kinachochangia katika kukusaidia kutimiza malengo yako.Kumbuka kuwa kiwango cha maarifa uliyonayo ndicho kinatengeneza kiwango cha mafanikio utakayopata katika malengo uliyojiwekea.Weka bajeti yako maalumu ya kununua vitu ambavyo vinakusaidia.Pia jilazimishe kutumia muda wako katika kujijenga zaidi na sio katika kujiburudisha.Kama wewe unaweza kushinda kwenye televisheni masaa mawili ama kuchart kwenye facebook ama watsapp lisaa lizima lakini huwezi kutumia hata nusu saa kujisomea kitabu basi ujue bado uko mbali na mafanikio.Hebu jaribu sasa kuweka mkakati wa namna ambavyo utakuwa unaongeza maarifa kila siku ili kufanikisha malengo yako.
• ANZA LEO,ANZA SASA
Kati ya vitu hatari sana kuelekea katika mafanikio yako ni ile hali ya kughairisha mambo kila wakati.Kuna watu wengi sana wakati mwaka huu unaanza walijiwekea mipango mingi sana lakini hadi leo hawajaanza hata mpango mmoja kati ya hiyo(sina uhakika kama na wewe ni mmoja wao).Tatizo la kughairisha kuanza limewafanya watu wengi sana washindwe kufanikiwa katika maisha yao.
Watu wengi ukiwauliza sababu za wao kutoanza yale mambo ambayo wanayatamani kuyafanya watakupa visingizio vya kuwa mazingira hayaruhusu,bado hawajapata mtaji,bado wanasubiri mtu wa kuwasapoti n.k.kama kweli unataka kufanikwia katika maisha yako ni lazime uwe mtu ambaye uko tayari kuanza pale ulipo kwa kutumia kile ulichonacho.Kila lengo ulilonalo lina hatua ambayo unaweza kuichukua kwa sasa.
Usiwe mtu ambaye kila wakati unasubiri kila kitu kiwe sawa ili uanze kuchukua hatua,hapana-Martin Luther King Jr aliwahi kusema-“Faith is taking the first step when you don’t see the whole staircase”(Imani ni kuanza kupanda ngazi ya kwanza hata kama hauoni mwisho wa ngazi unayopanda).Acha kuwa wale watu waanitwa “nitaanza kesho”(Mr/Mrs.Tommorow)-Wewe kila siku ukikutana na wenzako wakikuuliza kuhusu malengo yako,kazi yako ni kusema nitaanza kesho.Jitahidi uanze kutekeleza wazo lako kuanzia leo.
Kama ujumbe huu umekuwa na manufaa kwako,basi tafadhali utume kwa wengine ili waweze kufaidika nao pia.
Siku zote kumbuka kuwa mafanikio yanapatika kwa wale watu ambao wako tayari kuzingatia mambo hayo hapo juu.Kama ungependa kupata mafundisho ya namna hii kila siku basi unaweza kutembelea na kulike ukurasa wangu wa facebook(Joel Nanauka) au instagram (joel_nanauka) na utapata mafundisho ya kukusaidia kuifanikisha ndoto yako kila siku.Pia unaweza kujiunga na madarasa kwa njia ya WATSAPP kwa kutuma neno “NDOTO YANGU” ikifuatiwa na jina lako kamili kwenda 0655 720197 na utaunganishwa na hakuna gharama yoyote ile utakayotozwa.
Kama ungependa kupata ushauri zaidi kuhusu namna ya kutimiza malengo yako ama ungependa kunieleza Makala hii ilivyokusaidia,tafadhali tuwasiliane kwa barua pepe(jnanauka@gmail.com ama kwa simu 0743 868507 au tembelea tovuti yangu www.JoelNanauka.Com).
See You At The Top
Joel Nanauka

No comments:

Post a Comment