.

.

.

.

Wednesday

Radi yapiga kanisa, yaua watu watano

Watu watano wamefariki dunia papo hapo katika kijiji cha Shilabela, kata ya Bwanga, wilayani Chato, mkoa wa Geita, baada ya kupigwa na radi wakati wakiendelea na ibada ya Sikukuu ya Pasaka.

Tukio hilo lilitokea juzi jioni kwenye Kanisa la Assemblies of God Tanzania (AGT) na kujeruhi watu wengine 18 wakati wakiwa kwenye maadhimisho ya sikukuu ya kufufuka kwa Yesu Kristo, Pasaka. Kati ya majeruhi hao, wanne wamelazwa katika Zahanati ya Bwanga, wilayani Chato.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, akizungumza na NIPASHE jana, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataja waliofariki ni Daud Merdad (20), Daud Lazaro (20), Saimon Marco (15), Haile Shija (20) na Monica Sumuni (19).

Kamanda Konyo aliwataja majeruhi watatu waliolazwa Zahanati ya Bwanga ni Mabula Mathias (8), Fabian Ezekiel (10) na Edina Leonard (21).

Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, Deogratias John, alisema majeruhi 18 walipokelewa katika zahanati hiyo, lakini 14 walitibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya hali zao kutengemaa.

Akizungumzia tukio hilo, Diwani wa kata hiyo, Mahobe Chiza, alisema ni kubwa na la aina yake lililotokea wakati wananchi hao wakisherehekea sikukuu ya Pasaka.

“Walikuwa katika sikukuu ya Pasaka, lakini bahati mbaya mvua iliyokuwa ikinyesha ilisababisha radi kupiga na kuwadhuru waumini hao,” alisema Chiza.

Naye Mchungaji wa kanisa hilo, Deus Mhangwa, alisema kanisa lake limepata msiba mkubwa wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya Pasaka, ambayo ni siku ya kukumbuka kufufuka kwa Yesu Kristo baada ya kusulubiwa msalabani.

“Kila nafsi itaonja mauti, lakini tukio hili limewaachia simanzi kubwa waumini wa kanisa pamoja na wananchi kutokana na kupotea kwa nguvu kazi ya kanisa na taifa kwa ujumla,” alisema  Mchungaji Mhangwa.

No comments:

Post a Comment