.

.

.

.

Saturday

Philip Mangula awavaa maaskofu kuhusu mahakama ya kadhi katika Katiba mpya.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula, amewajia juu baadhi ya viongozi wa dini kwamba wanawapotosha wananchi waikatae Katiba inayopendekezwa kwa kuwa inapendekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.

Mangula amesema kuwa katiba hiyo haina ibara inayozungumzia masuala ya dini na Mahakama ya Kadhi na kuwataka wamuonyeshe kipengele kinachotaja masuala hayo.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula.
 Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanafunzi wa sekondari, wanachuo na walimu wa Shule ya Sekondari Hagaf.

Mangula alifafanua kuwa ameisoma Katiba yote na hajaona ibara wala sura inayozungumzia masuala ya udini wala Mahakama ya Kadhi.

 Mangula alisema kuwa viongozi wa dini wanawaelekeza wananchi kuikataa katiba hiyo, lakini walichofanya maaskofu ni kutoa matamko ya kupinga kuwasilishwa bungeni na kupitishwa kwa muswada wa kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.Maelekezo yao kwa waumini wao kutokuipigia Katiba kura ya ndiyo, yalitokana na kutoridhishwa kwa viongozi hao na mchakato mzima ikiwamo kusuasua kwa uandikishaji wa wapigakura, kuchelewa kupelekwa kwa nakala za Katiba na mgawanyiko katika Bunge Maalum la Katiba.

“Katiba hii inayopendekezwa nimeisoma yote, lakini sijaona mahali hata panapozungumzia masuala ya dini fulani, lakini nashangaa katika makanisa wananchi wanashawishiwa kutoipigia kura kwa sababu inaunga mkono Mahakama ya Kadhi, hakuna kitu kama hicho,” alisema Mangula.

 Alisema alikuwa katika kanisa moja anakosali na Mchungaji aliwaeleza waumini wasiipigie kura Katiba inayopendekezwa kwa kuwa ina masuala ya Mahakama ya Kadhi na kwamba alipomuuliza ni ibara gani inayozungumzia mahakama hiyo, mchungaji huyo alishindwa kuitaja na kusema haifahamu.

 “Jumapili moja kanisani, Mchungaji aliwahimiza wananchi kijiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura na wasiipigie Katiba inayopendekezwa kura ya ndiyo kwa sababu katika katiba hiyo kuna masuala ya udini na Mahakama ya Kadhi. Lakini nilipomuuliza alisema kuwa yeye kasoma waraka na Katiba bado hajaisoma na akawa anashangaa kama kipengele kimo ama hakimo,” alisema Mangula. 

Mangula aliwaeleza walimu na wanafunzi hao kuwa kiongozi yeyote atakayewataka kutoipigia kura katiba hiyo kwa maelezo kuwa ina mrengo wa dini fulani, wamwambie aeleze ni ibara gani inayozungumzia suala hilo.

 Alisema anawashangaa wanaowashawishi wananchi kutoipigia kura katiba hiyo wakati hawajaisoma na kuelewa mambo yaliyomo. 
Alisema kilichomo katika Katiba hiyo ni ibara inayozungumzia utawala wa sheria na kuwapo kwa Mahakama huru.

 Alisema kuwa kuna ibara inayoeleza kuwa Jamhuri ya Tanzania itakuwa na utawala wa sheria na huru isiyofungamana na dini yoyote.

“Watu wameanza kuzua mambo ya ajabu sana na wanaizuia Katiba, Katiba hii inasema Tanzania itakuwa ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na utawala wa sheria, inayojitegemea na isiyo fungamana na dini yoyote,” alisema Mangula na kuongeza:

“Anza ukurasa wa kwanza mpaka wa mwisho, hakuna sehemu inayozungumzia Mahakama ya Kadhi,” alisisitiza. 

 Alisema katiba hiyo ina mambo mengi mapya tofauti na ya zamani kama ufafanuzi wa makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 na kuwa makubaliano hayo ndiyo msingi wa nchi.

 Alisema kuwa katika Katiba inayopendekezwa, kuna misingi ya utawala bora na umiliki wa ardhi na kuwa ardhi hiyo inatunzwa na mali ya Mtanzania wa kizazi cha sasa na cha baadaye. 

Katika hatua nyingine, Mangula alikubaliana na kauli ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kuwataka viongozi wa dini kutowaelekeza wananchi wapige kura ya aina gani, bali waachwe wafanye maamuzi yao.

 Alisema kuwa wananchi wakiisoma Katiba inayopendekezwa kama kuna mapungufu watayaona na kama kuikataa, basi wafanye hivyo wenyewe.

Mangula aliongeza kuwa kwa wanaosema Katiba inayopendekezwa ipigiwe kura ya hapana, watoe hoja badala ya kutoa maelekezo bila kuwa na hoja zisizo na mashiko.

Jukwaa la Kikristo Tanzania linaloundwa na Baraza la Maaskofu (Tec), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Makanisa ya Pentekoste Tanzania (PCT), limekuwa likitoa matamko kadhaa ya kupinga kuwapo kwa Mahakama ya kadhi nchini.

Muswada huo hadi sasa umeshindikana kuwasilishwa bungeni katika mkutano wa 18 na 19 baada ya wabunge kugawanyika wakati wa semina ya kuujadili. 

SOURCE: NIPASHE

No comments:

Post a Comment