.

.

.

.

Tuesday

Askofu aeleza changamoto sera mpya ya elimu nchini

Siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kuzindua sera mpya ya elimu nchini na kusisitiza kuwa serikali itaweka sawa viwango vya utozaji wa ada kwa shule binafsi nchini, Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fedrick Shoo, amesema serikali inaweza kufanikisha mpango huo, lakini hatma ya kukua au kuporomoka kwa sekta hiyo ipo mikononi mwa wadau.

Alisema suala hilo linapaswa kuwashirikisha wadau wote, kwa kuwa wadau hao, wamekuwa kitovu cha elimu kwa miaka mingi, hata kama serikali imejipanga kufanya utafiti wa kina kukabiliana na changamoto hiyo, kabla ya kupanga na kutangaza viwango elekezi vya utozaji wa ada.

Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fedrick Shoo.
Dk. Shoo alikuwa akizungumza juzi katika Shule ya Sekondari ya Mtakuja iliyopo Kata ya, Wilaya ya Moshi wakati wa uzinduzi wa masomo kwa njia ya ‘tablets’, mpango ambao KKKT imeeleza kwamba unalenga kuchochea wanafunzi kuyapenda na kuyasoma masomo ya Sayansi.

“Sera mpya ya elimu iliyozinduliwa, naamini itamaliza udhaifu uliokuwa ukipigiwa kelele na wadau kwa miaka mingi sasa, ikiwamo suala la mitaala, lakini kama taifa, tuanze kuthamini juhudi za marafiki wa elimu wanaotuunga mkono,” alisema.

Alisema Taasisi ya Opportunity Education Foundation (OEF)ya Marekani,  imeamua kuwekeza katika mikoa 10 ya Tanzania, ikivutiamasomo ya Sayansi.

Alisema mpango huo wa kuvutia wanafunzi kupenda zaidi masomo ya Hisabati, Biolojia aio, Kemia, Kiingereza, Jiografia na Historia, unalenga kuongeza kiwango cha ufaulu na idadi ya wataalam katika fani hizo.

Mkuu wa Shule hiyo, Emanuel Lyatuu, aliwaeleza wadau wa elimu mkoani kuwa masomo hayo yatafundishwa kwa njia ya elektroniki tofauti na ilivyozoeleka ubaoni na kwamba wanafunzi watalazimika kufanya mitihani yao ya muhula kwa njia ya mtandao. Taasisi hiyo ya Marekani imeipatia tablets 65.

Ofisa Mipango wa OEF, Juliana Bwire, alizitaja shule 10 za Sekondari zilizochaguliwa nchini kuingia katika mpango wa majaribio wa miaka miwili kuwa ni Mtakuja (Kilimanjaro), Ilboru wanaume na Peace House (Arusha), Bwiru wanaume (Mwanza), Mzumbe (Morogoro) na Wama (Rufiji).

Nyingine ni Josaya wanawake (Bukoba), Msalato wanawake (Dodoma), Fidel Castro (Pemba) na Shule ya Sekondari ya Mchepuo wa Kiingereza ya Loleti (Zanzibar).

Mwakilishi Mkazi wa Taasisi hiyo nchini, Mchungaji Martin Russel, alisema kuwa OEF imekuja na teknolojia mpya iliyoboreshwa zaidi duniani ya kuvutia masomo ya Sayansi kwa kutumia video 733 ambazo zinatumika kukuza uelewa wa mwanafunzi darasani.

Source:ippmedia

No comments:

Post a Comment