.

.

.

.

Saturday

VIFUNGO, MATESO NA NIRA ZA SHETANI KATIKA MAISHA YA MWAMINI.

umapili iliyopita tulianza kuangalia kwanini watu waliyookoka, wanaomwamini Bwana na kumpenda Yesu maishani mwao wanateseka na kufungwa na adui katika maeneo mbali mbali ya maisha yao.
Tulisema zipo sababu kuu mbili kwanini watu wa Mungu huwa wanafungwa na kuteswa na adui katika maisha yao.

1. Kuna kweli wasiyoijua ambayo inampa adui mwanya wa kuwatesa na kuwasumbua. Kazi hizi za adui ambazo zinatokea katika maisha ya waamini kwa sababu hawajui tunaziiita uonevu na ni kazi za adui zisizo halali katika maisha ya mwamini.

2. Uhalali ambao shetani anapewa katika maisha ya mwamini kwa sababu ya mlango ambao mwamini anaufungua kupitia aina ya maisha anayoishi kimwenendo na kitabia.
Katika sababu ya kwanza ambayo inatoa mwanya kwa adui kuyatesa na kuyasumbua na kuyafunga maisha ya mtu, maandiko yanatuambia:
Isaya 5: 13.
13Kwa sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa; na watu wao wenye cheo wana njaa, na wengi wao waona kiu sana. 

Ni wazi kutokana na huu mstari, watu wa Mungu wanachukuliwa mateka kwa kukosa kuwa na maarifa.
Shetani anatumia huo mwanya wa watu wa Mungu kutokuwa na maarifa sahihi ya neno la Mungu na maagano ya Mungu kuwateka watu wa Mungu na kuwaweka chini ya ulinzi.
Ndo maana kitu cha kwanza cha muhimu kwa watu wa Mungu baada tu ya kuokoka, baada tu ya kuamini na kumfanya Yesu Bwana na Mwokozi wa maisha yao ni kukua katika kumjua Mungu na neno Lake.
Maandiko yanatuambia:

Yohana 8: 31, 32, 36.
31Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; 32tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru. 36Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli. 

Ni wazi kuwa baada ya kumwamini Yesu yatupasa kukaa katika neno Lake na tutakapoendelea kukaa katika neno Lake tutaifahamu kweli na hiyo kweli tutakayoifahamu itatuweka huru.

Mtu anayewekwa huru ni mtu ambaye kabla ya hapo alikuwa kifungoni ila kilichokuwa kinapelekea huyu mtu aendelee kuwepo kifungoni na kunyanyaswa na adui ni kutojua kweli ya Mungu kwa habari ya kile ambacho Yesu tayari amefanya kwa ajili yake.

Pindi anapojua, ile kweli inamweka huru na hayo manyanyaso ya adui katika maisha yake.
Yesu huwaweka huru watu Wake kwa kweli ya neno Lake, na akiwaweka huru kwa hiyo kweli wanakuwa huru kweli kweli.
Maandiko yanaendelea kutuambia sehemu nyingine:

Wagalatia 5: 1.
1 Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa.
Kristo alishatuweka huru na huo uhuru ambao tumewekwa huru na Yesu umeshaandikwa katika maandiko. Sasa tusipojua uhuru tuliyoandikiwa ni ngumu sana kusimama katika huo na adui anatumia huo mwanya kutunasa na kutuweka chini ya kongwa la utumwa.
Tunasoma katika maandiko:

Wagalatia 4: 1.
1Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote; 
Upo utumwa katika maisha ya mwamini ambao ni matokeo ya utoto.
Sasa utoto kiroho sio matokeo ya ameokoka lini bali ni matokeo ya hajui nini.

Tunakua katika Kristo kwa kadiri ufahamu wetu unavyofunguliwa kuijua kweli.
Nataka tuangalie picha mbili za kimaandiko Jumapili hii ya leo ili tuelewe jinsi ambavyo kweli ya Mungu ina nafasi kubwa sana ya kumweka mtu na bila hiyo kweli kuwepo mtu anaweza akawa huru tayari asijue akaendelea kuishi kana kwamba amefungwa.

Matendo 12: 1 - 12.
1 Panapo majira yale yale Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa. 2Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga. 3Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi akaendelea akamshika na Petro. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa. 4Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu.

5 Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. 6 Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa analala katikati ya askari wawili, amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakailinda gereza. 7Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi. 8Malaika akamwambia, Jifunge, kavae viatu vyako. 

Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, Jivike nguo yako, ukanifuate. 9Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono. 10Na walipopita lindo la kwanza na la pili, wakaja hata mlango wa chuma wa kuingilia mjini, ukawafungukia wenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha. 11Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi. 
Maandiko yanatuambia jinsi Herode alivyoanza kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa. Alimwua Yakobo ndugu yake Yohana kwa upanga.

Akaenda hatua zaidi akamshika na Petro amkamweka gerezani na kumtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne ili wamlinde ili amtoe na kumweka mbele ya watu baada ya pasaka kupita.
Petro akiwa analindwa vikali gerezani, kanisa likaomba kwa juhudi kwa ajili yake.

Ile siku ambaye Herode alitaka kumtoa, usiku huo akiwa amelala kati ya askari amefungwa minyororo miwili walinzi mbele ya mlango wakiilinda gereza, malaika wa Bwana akasimama karibu naye na nuru ikamulika mule chumbani.

Unaweza ukawa kifungoni na ukawa unaomba au unaombewa kwa bidii ili utoke katika hicho kifungo. 
Njia ya Mungu ya kukutoa kwenye hicho kifungo ni kutuma malaika ambaye akija nuru itamulika katika gereza lako.

Embu tutafute kujua huyu malaika ni nani?
Ayubu 33: 23.
23 Kwamba akiwapo malaika pamoja naye,

Mkalimani, mmoja katika elfu,
Ili kumwonyesha binadamu hayo yampasayo;

Huyu malaika ni mkalimani. Mtu ambaye anatusaidia kujua maana ya neno.
Hawa ni watu waliyopakwa mafuta na Mungu kulifungua neno la Mungu kwetu kwa njia ya mahubiri na mafundisho.

Wanapolifungua neno la Mungu kwetu nuru inatujia katika magereza yetu kama Petro nuru ilivyomjia kwenye gereza Lake.
Zaburi 119: 130.

130 Kufafanusha maneno yako kwatia nuru,
Na kumfahamisha mjinga.
Mkalimani ni mtu ambaye anafafanusha maneno ya Mungu na anapoyafafanusha, nuru inaachiliwa katika maisha yetu na hiyo nuru ikija gerezani mwetu yanaanza kutokea kwetu yaliyotokea kwa Petro.
Hawa wakalimani ni mitume, manabii, wainjilisti, wachungaji na waalimu ambao wanapewa hiyo neema ili kufafanusha maneno ya Mungu tuyaelewe na tukielewa mwanga unakuja kwetu.
Maandiko yanatuambia:

Yohana 1: 4, 5.
4Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. 5Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.
Ndani ya neno mna uzima na huo uzima ni nuru ya watu. Huo uzima ukiachiliwa kwa njia ya kufafanusha maneno ya Mungu, inatupa nuru ya kuangaza kwenye giza letu na hakuna giza litatuweza.
Wengi wanaendelea kukaa chini kwenye vifungo vyao na mateso yao kwa sababu mwanga sahihi wa neno la Mungu haujawafikia.

Isaya 60: 1, 2.
1 Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja,
Na utukufu wa BWANA umekuzukia.
2Maana, tazama, giza litaifunika dunia,
Na giza kuu litazifunika kabila za watu;
Bali BWANA atakuzukia wewe,

Na utukufu wake utaonekana juu yako.
Bila nuru yako kuja huwezi kuondoka hapo ulipo na kuangaza.
Nuru yako, ufahamu wa neno lako kutoka kwa Mungu ndo sababisho la kuondoka kwako pale ulipo na kuangaza.
Hawa wakalimani wanashiriki katika kuleta kwetu nuru ya neno la Mungu ili tutoke kwenye vifungo vya adui maishani mwetu.

Kitu cha ajabu ambacho tunakiona pale gerezani kwa Petro, yule malaika alipokuja hakuhangaika na gereza, wala lango la gereza, wala walinzi, wala minyoro ya Petro, yeye alishughulika na Petro.
Once ukiokoka, shida sio shetani na kazi zake, shida ni wewe. Kuna mwanga ambao huna ambao unakuzuia kutembea katika uhuru ambao Kristo amekukusudia.
Baada ya yule malaika kuja pale gerezani na nuru kuingia mule, alimpiga Petro ubavuni na kumwamsha kutoka katika usingizi.

Kuna namna ambayo nuru ya neno la Mungu inakuja maishani mwetu na kutushtua kutoka hali ya kujisahau na kutuamsha toka katika usingizi wetu.
Maandiko yanasema:

Waefeso 5: 14.
14Hivyo husema,
Amka, wewe usinziaye,
Ufufuke katika wafu,
Na Kristo atakuangaza.
Ilihitajika Petro aamke ili ile nuru iliyoingia ndani ya lile gereza imsaidie kutoka katika hilo gereza.
Yule malaika alimpa maelekezo Petro akaitika na kufanya alivyoelekezwa na katika kufanya alichoelekezwa, minyororo yake ikamwanguka mikononi yenyewe.

Huwa tunahangaika bure na minyororo na kuwa na ibada maalum za kukata minyororo ya adui katika maisha ya watu wakakti kinachohitajika ni nuru na maelekezo ambayo mtu akifuata minyororo inaachia yenyewe.
Wakaondoka wakalipita lindo la kwanza na la pili la askari na wala hao askari hawakuweza kufanya kitu maana Petro anaondoka na kuangaza kwa kuwa nuru yake imekuja na walipofika kwenye lango la kuingia mjini liliwafungukia lenyewe bila hata kufanywa kitu.

Nuru, ufahamu; una nguvu kubwa ajabu kufungua na kuweka mtu huru lakini pia ujinga na kutokujua kuna nguvu kubwa mno kumfunga mtu na kumweka katika hali ya mateso na vifungo visivyokoma.
Kila mmoja wetu aliyeokoka tayari yupo huru lakini tusipojua kuwa tupo huru tutaendelea kukaa katika hali ya kufungwa japo tayari magereza yetu yamefunguka na vifungo vyetu vilisha achia.

Matendo 16: 25 - 30.
25Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. 26Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa. 27Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia. 28Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa. 29Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila; 30kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? 

Wakati Paulo na Sila walipokuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za sifa kuna tetemeko kuu la nchi lilitokea, misingi ya gereza ikatikisika, milango ya gereza ikafunguka na vifungo vya wote vikalegezwa ila hawakuweza kutoka humo gerezani kwa kuwa hapakuwa na mwanga.

Unaweza ukawa huru lakini kama hujui utaendelea kuteswa na kuonewa na kunyanyaswa na adui.
Ila ukijua kweli hiyo kweli unayojua inakuweka huru na kila uonevu na kila manyanyaso ya adui.
Juma lijalo tutaenda sasa kuangalia sababu ya pili inayopelekea watu wa Mungu kuteswa, kufungwa na kunewa na adui.
Mungu akubariki sana.

No comments:

Post a Comment