.

.

.

.

Wednesday

Umeme wasababisha kifo cha watoto kanisani kwa Askofu Gwajima

Watoto wawili ambao ni ndugu, wamefariki dunia katika Kanisa la Ufufuo na Uzima, linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, jijini Dar es Salaam.

Watoto hao walifariki dunia kutokana na kupigwa na shoti ya umeme wakiwa katika ibada juzi.

Tukio hilo lilitokea wakati watoto hao wakiwa na waumini wengine wakifuatilia ibada ya kufunga ndoa.

Inadaiwa kuwa, watoto hao walipigwa na shoti baada ya kukanyaga nyaya za umeme wakati wao na waumini wengine walipoamka vitini kwenda kuwapokea maharusi wakati wakiingia kanisani hapo.

BABA ATILIA SHAKA
Hata hivyo, baba mzazi wa watoto hao, David Oturo, ameonyesha hali ya wasiwasi na kutokukubalina na mazingira ya vifo vya watoto wake, Sarah (10), Goodluck (4) na kusema ni vifo vya utatanishi.

Akizungumza na chanzo cha habari hii jana kuhusiana na vifo hivyo alieleza kuwa, Sarah alikuwa anasoma Shule ya Msingi Milambo iliyopo Mbezi Juu darasa la nne na Goodluck alikuwa anasoma chekechea ya Ushindi.

Alisema siku hiyo kulikuwapo na watoto wengi waliokusanyika katika viwanja vya kanisa hilo, lakini ni watoto wake tu ndiyo waliofikwa na mauti huo.

“Pale kanisani kulikuwa na watoto wengi na waumini wengine lakini kwanini imetokea kwa watoto wangu tu?” alihoji.
Aliongeza kuwa kabla ya kukutwa na mauti jioni, majira ya mchana, Sarah aling’atwa na nyuki sehemu ya mguuni waliotokea katika kanisa hilo ghafla.

Alisema ilipofika jioni ndipo watoto wake peke yao walikanyaga nyaya za umeme zilizokuwa zimepitishwa katika viwanja hivyo.

Oturo alifafanua kuwa nyanya hizo za umeme hazikuwa zimechunika wala hazikuwa na dalili ya kuwa na hitilafu.

“Sehemu yenyewe haikuwa na mchubuko wowote wa waya, wala hakukuwa na hitilafu yoyote, ilikuwa ni sehemu ambayo inaonekana imetengenezwa na mtu ambaye ni mtaalam wa masuala ya umeme,” alisema Oturo.

Alisema watoto hao walikuwa na mama yao ambaye ndiye anayekweda nao kila siku ya Jumapili katika ibada.

Oturo aliongeza kuwa, baada ya watoto wake kupigwa na shoti ya umeme, walipewa huduma ya kwanza na uongozi wa kanisa hilo na kisha kukimbizwa katika Hospitali ya TMJ.

Akielezea huku akionekana kuwa na huzuni, Oturo alisema baada ya kufikishwa katika hospitali hiyo, walipelekwa katika hospitali ya Mwananyamala na ndiko mauti yalipowafikia.

“Sehemu yoyote kunapokuwa na shoti lazima fundi umeme atakuwapo, lakini kitu cha kushangaza kwa nini imewakuta watoto wangu tu, wakati kulikuwapo na umati wa watu wengi?” alihoji baba wa watoto hao.

Alisema waliripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Kawe na kuandikiwa RB KW/RB/5374/2015.

Oturo alisema kwa sasa wanasubiri uchunguzi wa Jeshi la Polisi ili miili isafirishwe kuelekea Musoma, mkoani Mara kwa mazishi.

MASHUHUDA WASIMULIA
Baadhi ya mashuhuda waliokuwapo wakati wa  tukio hilo, Aida Simon na Sylvia Gozbert, walieleza kuwa siku ya tukio kulikuwa na harusi kanisani hapo.

Walisema maharusi walipokuwa wanaingia kanisani, Askofu akawaambia watoto na waumini kwenda kuwapokea na kuwashangilia maharusi hao.

Walisema ghafla wakati tukio hilo likiendelea ndipo watoto hao walipigwa na shoti ya umeme.

UONGOZI WA KANISA WAZUNGUMZA
Askofu wa Kanisa hilo, Josephat Gwajima, alisema kuwa tukio hilo lilitokea baada ya yeye kuondoka kanisani hapo.
Alisema ni kweli watoto hao walifariki kutokana na shoti ya umeme iliyotokea kanisani hapo.

“Kwa sasa sina taarifa kamili kwa sababu tukio lilitokea baada ya mimi kuondoka kanisani, lakini ni kweli watoto hao wamefariki na hivi sasa ninaelekea kanisani ambako nitapata taarifa kamili,” alisema Gwajima.

KAULI YA POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. Wambura alilieleza chanzo kuwa,  uchunguzi bado unaendelea wa kubaini kama ni kweli tukio hilo lilisababishwa na kukanyaga nyaya za umeme.

Alisema polisi pia wanachunguza kufahamu kama kuna  tukio la makusudi  ama kulikuwa na uzembe wowote uliosababisha kutokea kwa vifo hivyo.

“Baada ya uchunguzi huo kukamilika, ndipo tutajua ni hatua gani za kisheria tutakazozichukua kutokana na tukio hilo,” alisema Wambura.


CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment