Waandaaji wa Tamasha la Pasaka wamesema kuwa wamealika wadau mbalimbali wakiwemo mawaziri wote wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama ilieleza kuwa wanaamini tamasha la mwaka huu litakuwa la aina yake.
“Tumewaalika mawaziri wote. Mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bennard Membe, lakini na mawaziri wengine wote tumewaalika na wengi wamethibitisha watashiriki.
“Baadhi hawajathibitisha kwa vile walikuwa bungeni Dodoma, lakini mpaka leo jioni (jana) naamini wengi watakuwa wamethibitisha,” alisema Msama.
Pia alisema maandalizi ya tamasha hilo yanaenda vizuri na kuwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kufanikisha tamasha hilo ambalo litakuwa ni la aina yake.
Alisema waimbaji raia wa Afrika Kusini Rebbecca Malope na Sohly Mahlangu wanatarajiwa kuwasili Dar es Salaam kesho tayari kwa tamasha hilo. Muingereza Ifeanyi Kelechi na Mzambia Eiphraim Sekeleti wanatarajia kuwasili leo Ijumaa.
“Tamasha la mwaka huu lina mambo mengi ambayo yataendana na miaka 15 ya tamasha hilo kubwa hapa Tanzania kwa sababu linashirikisha waimbaji wa Kimataifa na viongozi wakubwa serikalini,” alisema Msama.
Alisema mwimbaji Mtanzania anayeishi Kenya, Faustine Munishi naye anatarajia kuwasili Dar es Salaam leo Ijumaa jioni tayari kwa tamasha hilo.
“Wasanii wamepania mambo makubwa sana kwenye tamasha, najua mashabiki watafurahi na mambo yatakavyokuwa,” alisema Msama, ambaye mwaka huu tamasha lake linatimiza miaka 15.
source:fullshangweblog
source:fullshangweblog
No comments:
Post a Comment