Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa, amemsimamisha kanisani Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na kuwaomba waumini waliokuwa wamehudhuria ibada ya Pasaka katika Kanisa la Azania Front jijini Dar es Salaam kumpigia makofi kutokana na kazi nzuri anayoifanya katika wizara yake, huku akimtaka kuwapuuza baadhi ya watu wanaombeza.
Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya Dk. Malasusa kumaliza kuhubiri katika ibada ya pili kanisani hapo jana.
Nyalandu ambaye alikuwa ameketi eneo la waimbaji kwaya ya kanisa alikuwa ameongozana na mke wake, Faraja Nyalandu, na watoto wake wawili, aliitikia ombi la Dk. Malasusa kwa kusimama pamoja na mke wake na kupigiwa makofi na waumini hao.
“Ninaona uwapo wa Waziri wa Maliasili na Utalii katika ibada hii, naona umeongozana na mke wake na watoto, nafahamu kwamba wewe ni mtumishi mzuri wa Mungu na hata ulivyokaa sehemu hiyo ya waimbaji hujakosea unastahili kukaa hapo kwa kuwa na wewe ni mwimbaji,” alisema Dk. Malasusa.
“Tunatambua jitihada na kazi nzuri unayofanya katika wizara yako, ninaomba uwapuuze baadhi ya watu wanaokubeza, sisi tunatambua mchango wako na tunaunga mkono kazi nzuri unayoifanya na tuko nyuma yako tunakuombea, simama utusalimie na ninaomba mumpigie makofi kwa kazi nzuri anayoifanya, endelea hivyo hivyo” alisema Askofu Malasusa.
Kwa upande wake, Nyalandu akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa ibada hiyo, alisema anashukuru kwa kauli ya Dk. Malasusa kwa niaba ya wafanyakazi wenzake katika wizara yake na kwamba kazi anayoifanya katika wizara hiyo anatekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema ataendelea kufanya kazi kwa bidii hususani katika kuendelea kupambana na majangili na kukomesha vitendo vya uhalifu wa nyara za serikali.
“Alichokisema Askofu ni kwamba sisi viongozi tusikubali kukatishwa tamaa na mtu yeyote katika kazi tunazofanya, mimi na wenzangu katika wizara yangu na sehemu nyingine tunapopambana kwenye rasilimali za nchi tunahitaji kuungwa mkono na kutiwa moyo na kila mtu,” alisema Nyalandu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment