.

.

.

.

Wednesday

Askofu Chimeledya: Kura ya maoni ingesababisha hasara.


Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Jacob Chimeledya, amesema kuahirishwa kwa upigaji kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa ni jambo zuri kwani lingeweza kulisababishia Taifa hasara kubwa na kutumia vibaya rasilimali za Watanzania.

Kauli hiyo aliitoa wakati akihubiri katika ibada iliyofanyika katika kanisa kuu la Watakatifu wote Vinghawe, mjini hapa.

Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Jacob Chimeledya.
“Naipongeza Tume ya Uchaguzi (Nec) chini ya kiongozi wake Jaji mstaafu Lubuva kwa kuweza kuahirisha upigaji kura ya maoni ambayo ingefanyika Aprili 30 mwaka huu, mimi naona ni jambo zuri kwani lingeweza kulisababishia Taifa hasara kubwa,” alisema Askofu Chimeledya.

Alisema pamoja na kuahirisha kazi hiyo ni vyema serikali ikarekebisha changamoto zote zilizojitokeza wakati wa uandikishaji wa daftari la kupigia kura ili kuweza kupunguza Watanzania wengi kukosa haki yao ya msingi na kikatiba.

 “Serikali ingefanya mapema suala la uandikishaji wa daftari la wapiga kura likamilike kabla ya Bunge kuvunjwa ili kuweza kuwapa Watanzania kutoa nafasi nzuri zaidi ya kujiandaa na uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu,” alisema.

Aidha, aliwataka viongozi wa serikali kujifunza kuwa katika mchakato mzima wa Katiba, upigaji kura umeshindwa kufanikiwa kutokana na kutokuwapo na maandalizi mazuri.

 Kuhusu rushwa, Chimeledya alisema vitendo vya rushwa na ufisadi vinaweza kuhatarisha amani ya nchi kutokana na watu kukosa imani na viongozi wao. 

Alisema vitendo hivyo vinasababisha Watanzania wanyonge wanakufa kwa kukosa dawa hospitalini, akina mama wanakufa kwa kukosa vifaa vya kujifungulia na watoto shuleni hawana vifaa vya kutosha.

Akizungumzia kuhusu mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), askofu Chimeledya alisema kila mtu ana haki ya kuishi kwa mujibu wa Katiba.

Alisema mbali na mauaji hayo pia kuna vitendo vingine nyuma ya pazia ambavyo vinatokana na watu kukosa hofu ya Mungu.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment