Wakati Rais Jakaya Kikwete akisema msimamo wa Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) wa kuwataka waumini wao kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa ni wa hasira pia usiokuwa na tija kwa maendeleo ya Taifa, baadhi ya maaskofu wameshikilia msimamo huo.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo juzi Jumamisi katika mkutano wa kamati ya amani ya Mkoa wa Dar es Salaam iliyoshirikisha wajumbe kutoka mikoa mbalimbali nchini unaowajumuisha viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo akilenga kuzungumzia tamko hilo la TCF walilolitoa Machi 12, mwaka huu.
Katika tamko hilo lililosainiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet liliwataka waumini wake kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura na kuipigia kura ya hapana Katiba hiyo.
Jukwaa hilo lilitaja sababu mbili za uamuzi wake huo kuwa ni Muswada wa Mahakama ya Kadhi kukiuka misingi ya Taifa kuwa na Serikali isiyo na dini na Kura ya Maoni kusababisha mgawanyiko.
“Hivyo basi, Jukwaa linawataka waumini wake wote wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, waisome Katiba Inayopendekezwa na kushiriki kikamilifu vipindi vya elimu juu ya Katiba Inayopendekezwa na kisha wajitokeze kwa wingi kupiga kura ya hapana,” lilisema tamko hilo.
Katika hotuba yake iliyodumu kwa saa 1.16, Rais Kikwete alianza kwa kuwaomba radhi viongozi hao kwa kuchelewa kwa akisema alikuwa na majukumu mengi. Mkutano huo ulikuwa uanze saa 3.00 asubuhi lakini Rais Kikwete alifika saa 6.30 mchana.
Alisema “Taifa linapitia hali isiyokuwa ya kawaida, tusipokuwa makini kuidhibiti itakuwa ni tatizo, ni kazi kubwa inayohitaji moyo, uvumilivu na viongozi wenye kujali masilahi ya Taifa.”
“Mwelekeo wa mambo hauhitaji uwe bingwa kujua hali hairidhishi sana na kama hatutachukua hatua hatuwezi kufika na tutasababisha uvunjifu wa amani za kidini na moto wake ni mkali sana,” aliongeza Rais Kikwete aliyekuwa akizungumza kwa umakini na taratibu.
Jukwaa la wakristo
Kuhusu tamko la Jukwaa la Wakristo, Rais Kikwete alisema wakati Taifa likisubiri kuona mchakato wa Katiba unakwenda hatua za mwisho kumekuwapo na matamko kadhaa ambayo hayakumfurahisha.
“Nimeyasoma matamko hayo yote kwa umakini, imenishangaza, imenisikitisha na kunihuzunisha. Siamini kwa nini wamefikia huko kwa kuunga au kutokuunga mkono,” alisema Rais Kikwete aliyekuwa akizungumza kwa sauti ya chini wakati wote wa hotuba yake.
“Kinachonisumbua ni kuipa sura na mtazamo wa kidini Katiba Inayopendekezwa, kama ingekuwa inakinzana na uhuru wa kuabudu hapo ingekuwa sawa lakini ibara ya 41 inatambua uhuru wa kuabudu na kuitangaza dini, sasa katika mazingira hayo kuwaeleza waumini kuikataa inanipa tabu sana,” aliongeza.
Alisema, “Katiba hii imezingatia na kutambua makundi mbalimbali na mimi sina haya kuwaeleza kuwa tuipitishe kwani licha ya upungufu ilionao, haifikii hii ya sasa. Tusipoipitisha tutaendelea kuitumia hii na sidhani kama kuna Rais atakuja na kuanza na mchakato wa Katiba, hivyo hii hii tuipitisheni kama ina upungufu utafanyiwa maboresho kwani Katiba siyo Msahafu au Biblia.”
Rais Kikwete anayemaliza muda wake wa uongozi mwaka huu alisema: “Waacheni waumini waamue Katiba wanayoitaka wao, hayo matamko niliyoyasoma yamejaa hasira kwa Serikali kupeleka bungeni Muswada wa Mahakama ya Kadhi.”
Katika kujenga hoja hiyo alisema Serikali imepeleka muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali ambao ndani kuna kifungu kinachohusu Mahakama ya Kadhi, jambo ambalo siyo geni kwa kuwa limekuwapo kwa kipindi kirefu.
“Tunachotaka kufanya ni kutambua hiki ambacho Waislamu wamekianzisha kwa kuwa na Mahakama ya Kadhi na makadhi, Serikali haitawasimamia wala kuziendesha mahakama hizo, hivyo hazina tatizo lolote,” alisema Rais Kikwete akitanguliza maneno kwamba, “naomba nitumie lugha ambazo sitowakwaza watu.”
“Siyo kila anachokitaka mtu kitakuwamo katika Katiba, mfano mimi na CCM tulikuwa na mambo 60 tuliyoyaona ya msingi sana yawemo katika Katiba lakini sidhani kama yanafika hata 12...kwa kuwa mchakato unaendeshwa kisheria basi tuuache umalizike kisheria,” aliongeza.
“Sidhani mnachokifanya ni sawasawa, mnawakwaza waumini wenu, waacheni waamue wao wenyewe kwani mkiendelea hivyo watawaona ninyi hamfai kwani kila mtu katika hili ana msimamo wake, mwingine anaona hili linafaa mwingine anaona halifai.”
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhadi Mussa Salum ambaye pia ni Sheikh wa mkoa huo, alisema wameamua kumwalika Rais Kikwete kuzungumzia na viongozi hao kutokana na Taifa kuwa katika hali ya sintofahamu.
“Tumeamua kukualika wewe uzungumze na viongozi wa dini zote zitakazosaidia kubadilisha hali iliyopo sasa. Umevumilia mengi kama Watanzania walikuudhi na kukukera kwa niaba yao uwasamehe,” alisema Sheikh Salum.
Naye Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Askofu Valentino Mokiwa alisema baada ya mkutano huo kuwa kuna umuhimu wa kutafakari mambo yanayosumbua na kuendelea kusumbua sana.
“Bado sijajua kama hotuba yake (Rais) aliyoitoa itatoa dira ya mchakato huu wa Katiba, tusubiri kuona kipi wananchi wataamua,” alisema Askofu Mokiwa ambaye pia ni Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Dar es Salaam.
Umoja wa makanisa Tanga
Katika tamko lake Umoja wa Makanisa Mkoa wa Tanga pamoja na kuwataka Watanzania kuikataa Katiba Inayopendekezwa, umeishauri Serikali kusogeza mbele Kura ya Maoni.
Msimamo huo ulitangazwa na Mwenyekiti wa umoja huo, Askofu Dk Jotham Mwakimage aliyezungumza na waandishi wa habari baada kikao cha maaskofu na wachungaji wa makanisa mbalimbali ya Tanga.
Alisema kikao chao kilichofanyika wiki iliyopita katika Kanisa la Agape jijini Tanga na kuhitimishwa jana, kimeamua kutambua na kuheshimu tamko la Jukwaa la Wakristo lililotolewa Machi 10, mwaka huu la kuwaomba Watanzania waipigie kura ya ‘Hapana’ Katiba Inayopendekezwa.
Sababu za kuikataa
Alisema Katiba hiyo ni imeligawa Taifa la Tanzania, iliandaliwa na kupitishwa kwa hila na kimabavu na ndiyo sababu inalazimishwa ipigiwe kura ya ‘Ndiyo’ bila kuruhusu masahihisho ya makosa yaliyomo.
Sababu nyingine kwa mujibu wa tamko hilo ni kwamba Katiba Inayopendekezwa iliandaliwa kwa hila ikiwa na madhumuni ya kuondoa Rasimu ya Katiba iliyotokana na mawazo ya wananchi walio wengi yaliyokusanywa na kuratibiwa na Tume ya Jaji Warioba.
“Walioleta msukumo wa kupitisha Katiba kimabavu, ndiyo wanaochochea uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi ili kuigawa nchi kidini,” alisema Mwakimage wakati akielezea sababu ya nne ya kutounga mkono katiba pendekezwa.
Umoja huo wa makanisha umesema katika tamko hilo kwamba ili kuondoa mkanganyiko, unaishauri Serikali kusogeza mbele Kura ya Maoni kwa sababu muda wa mwezi mmoja hautoshi kwa wananchi kuisoma, pia nakala zilizotolewa ni chache.
Sababu nyingine ya kupendekeza kusogezwa mbele kwa Kura ya Maoni ni kutoa nafasi ya kutosha ya kuboresha Daftari la Wapigakura na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
“Sisi umoja wa makanisa tunasisitiza kuwa Watanzania wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura na kupigia Katiba Inayopendekezwa kura ya Hapana, sawa na tamko la maaskofu,” alisema Mwakimage.
Baraza la makanisa
Wakati huohuo, Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) limetoa tamko kuhusu hali ya kisiasa nchini likiwamo suala la Katiba Inayopendekezwa,
Mahakama ya Kadhi na kusisitiza uamuzi wa kuwataka Wakristo kujiandikisha kwa wingi na kuipigia kura ya ‘Hapana’ katiba hiyo.
Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu CPCT, Askofu David Batenzi alitoa tamko hilo jana katika Kanisa la Bethel jijini Arusha mbele ya maaskofu wakuu 70 waliohudhuria na kujadili pamoja na mambo mengine, hali ya kisiasa nchini, akisema wamefikia hatua ya kutoa tamko hilo ili kuondoa mkanganyiko uliokuwapo.
Akifafanua mkanganyiko huo, Askofu Batenzi alisema kumekuwapo madai ambayo siyo ya kweli kuwa miongoni mwao kuna maaskofu wanaonyesha nia ya kuwaunga mkono wagombea urais na wengine wanatoa matamko kinzani dhidi ya tamko la Jukwaa la Wakristo (TCF), chombo ambacho CPCT ni mwanachama.
Askofu Batenzi alisema kuwa CPCT haina chama wala mgombea na kwamba wanaamini katika kumwomba Mungu awape kiongozi atakayelifaa Taifa.
“Mtu yeyote anayedai kuwa ni Mpentekoste aliyetenda au atakayetenda kinyume na msimamo huu, hakutumwa na wala hatakuwa ametumwa na CPCT,” alisema.
Alisema uwakilishi wa viongozi na wajumbe wa CPCT kwenye kikao cha TCF kilichotoa tamko, ulikuwa na baraka zote za baraza hilo na madai yoyote kwamba CPCT inaburuzwa na mwenyekiti na katibu wake kwenye tamko hilo yapuuzwe, kwa kuwa hayana msingi wowote.
Imeandikwa na Ibrahim Yamola (Dar), Burhani Yakub (Tanga) na Happy Lazaro, Arusha.
Source:mwananchi
No comments:
Post a Comment