Jeshi la Misri limefanya mashambulizi ya anga dhidi ya vituo vya Dola la Kiislamu nchini Libya, baada ya kundi hilo kusambaza video mtandaoni inayoonyesha Wakristo 21 kutoka Misri wakichinjwa.
Video iliyosambazwa mtandaoni na Dola la Kiislamu inaonyesha Wamisri 21 wakiwa wamevaa nguo za rangi ya chungwa na wakilazimishwa kupiga magoti ufukweni na kisha wakiuliwa mmoja mmoja. Rais wa Misri, Abdel Fatah al-Sisi ameahidi kuongeza nguvu katika kupambana na ugaidi. "Misri ina haki ya kulipiza kisasi kwa wauajia na wahalifu hao ambao hawana utu kabisa. Tutaamua wenyewe namna ya kulipiza kisasi na muda wa kufanya hivyo," amesema al-Sisi.
Jumatatu ndege za kijeshi za Misri zilifanya mashambulizi ya angani katika maficho ya Dola la Kiislamu nchini Libya nayo serikali ya al-Sisi imetangaza siku saba za kuomboleza vifo vya Wakristo hao waliokuwa waumini wa madhehebu ya koptik. Katika tamko lake uongozi wa kanisa la koptik umewataka waumini wake wawe na imani kwamba nchi yao haitatulia hadi pale ambapo waliofanya uasi huu watapewa adhabu wanayostahili.
Rais Abdel Fattah al-Sisi ameapa kulipiza kisasi |
Mwezi uliopita tawi la Dola la Kiislamu nchini Libya lilikuwa limetangaza kuwa limewateka nyara Wakristo 21 kutoka Misri na inaaminika kwamba hao ndio wanaoonekana kwenye video hiyo.
Misri kuwalinda raia wake Libya
Tangu kuangushwa kwa utawala wa Muamar Gaddafi mwaka 2011 maelfu ya vibarua wameelekea Libya kutafuta kazi na wengi wao wanatokea Misri. Hata hivyo Wakristo wa koptik mara kwa mara wamelengwa na mashambulizi yaliyofanywa na Waislamu wenye itikadi kali. Rais Abdel Fattah al-Sisi ameahidi kuhakikisha usalama wa wananchi wake walioko Libya. "Nimeiomba serikali iendelee kuwakataza Wamisri kusafiri kwenda Libya wakati huu mgumu ili kuokoa maisha yetu. Nimezitaka pia taasisi husika zichukue hatua kuwawezesha Wamisri warudi nchini mwao," alisema rais huyo.
Bunge la Libya limetoa salamu za rambirambi na kuitaka jumuiya ya kimataifa iiunge mkono Libya katika juhudi za kupambana na wanamgambo. Nao ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo umewataka Walibya wote wakatae vitendo vya Dola la Kiislamu. Rais Francois Hollande wa Ufaransa, ambaye alikuwa ameahidi kuiuzia Misri ndege za kijeshi, ameelezea wasiwasi wake juu ya kukua kwa Dola la Kiislamu.
Marekani kwa upande wake imelaani mauaji ya watu hao 21. Msemaji wa ikulu ya White House, Josh Earnest, amesema uovu wa Dola la Kiislamu usiojua mipaka unaiunganisha jumuiya ya kimataifa katika kulipiga kundi hilo.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp/ap
Mhariri: Daniel Gakuba
No comments:
Post a Comment