Askofu mpya wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo jana alitoa ujumbe mzito kwa Rais Jakaya Kikwete alipomtaka kuwawajibisha haraka wahusika kwenye kashfa ya escrow kwa kuwa “viporo vinaumiza tumbo”.
Dk Shoo aliyemrithi askofu Dk Martin Shao aliyestaafu, alitoa kauli hiyo mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika ambaye alimwakilisha Rais, wakati akihutubia kwenye ibada ya kuwekwa kwake wakfu na kusimikwa kwa msaidizi wake, Mchungaji Elingaya Saria iliyofanyika Usharika wa Moshi Mjini.
Mbali na Waziri Mkuchika, wengine waliokuwapo kwenye ibada hiyo ni mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu. Pia walikuwapo baadhi ya wabunge na maaskofu wa dayosisi 24.
Katika hotuba yake, Dk Shoo alisema kanisa linasikitishwa na ufisadi mkubwa unaoendelea miongoni mwa viongozi na watumishi wa umma na kiburi wanachokionyesha wanapoelezwa ukweli.
“Kinachotusikitisha zaidi ni wahusika kuonyesha jeuri kubwa na ukakamavu wa hali ya juu pale wanapoambiwa,” alisema Dk Shoo huku akishangiliwa.
“Mimi sioni mantiki kama mtu amehusika katika mambo fulani, halafu anaanza kusema sikueleweka vizuri halafu anajiuzulu.”
Ingawa hakumtaja kwa jina kiongozi huyo, Jaji Fredrick Werema alijiuzulu nafasi yake ya Mwanasheria Mkuu kwa kumwandikia barua Rais akieleza kuwa ushauri wake katika suala la escrow haukueleweka na umesababisha tafrani.
Katika sakata hilo la Escrow, Jaji Werema ndiye anayedaiwa kuandika barua akieleza kuwa fedha zilizokuwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow zilipwe IPTL bila ya kukatwa kodi.
“Tunatambua Rais ameanza kuchukua hatua dhidi ya watu kama hawa. Tunazidi kumwombea yeye na Serikali yetu ili wamwonyeshe hatua zaidi zinazofaa kuchukuliwa,” alisema Askofu Shoo.
“Panapohitajika kuchukua hatua, tusiweke viporo. Unajua viporo vikishakuwa vya muda mrefu, vinaumizaa tumbo,” alisisitiza Dk Shoo huku umati uliofurika ukilipuka kwa furaha na makofi.
Akitangaza uamuzi wake kuhusu maazimio ya Bunge la Muungano, Rais Kikwete alitangaza kumwondoa kazini Profesa Anna Tibaijuka, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, lakini akasema amemweka kiporo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Source:Mwananchi
No comments:
Post a Comment