.

.

.

.

Monday

Rais Kikwete: Bunge la Katiba lina Mapepo

Rais Jakaya Kikwete amewaomba Maaskofu na viongozi wengine mbalimbali wa dini nchini kuliombea Bunge Maalum la Katiba ili kuliondoshea mapepo yaliyosababisha vyama vinne kuvurugana na hivyo kutishia mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya.

Rais Kikwete alitoa ombi hilo kwa viongozi wa dini jana jijini Mbeya, katika hotuba yake aliyoitoa kwenye maadhimisho ya Jubilee ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Kanisa la Assemblies  of God (TAG), ambayo yaliadhimishwa kitaifa jijini hapo.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wananchi kwenye kilele cha sherehe za miaka 78 ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God, kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine,jijini Mbeya jana.picha ikulu
Alisema wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba walianza kutoelewana baada ya kufikia kipengele cha mjadala wa jumla kuhusiana na sura ya kwanza na ya sita ya rasimu ya katiba hiyo, wakati huo wakiwa tayari wameshaafikiana kwenye kamati na kujadili vipengele vilivyopo katika sura hizo na kutoka na maoni ya walio wengi na ya walio wachache.

“Hapa kuna mapepo ya kuombea, sasa TAG tusaidieni kuondoa pepo hili ili hawa waelewane warudi Bungeni wakapige kura,” alisema.

Kikwete alisema pepo aliingia baada ya kufikia hatua ya mjadala wa jumla na kwamba, kama vyama vikubwa vya CCM, Chadema, CUF na NCCR Mageuzi vitakubaliana, ana amini mambo yatakwenda vizuri katika mchakato wa Katiba.

“Maombi yangu kwenu viongozi wa dini... maaskofu, masheikh, manabii na maimamu, tuviombee hivi vyama vinne ili mazungumzo yao waliyoanza kuangalia namna ya kuendesha mchakato wa Katiba yaende vizuri na wafikie mwafaka warudi Bungeni kutupatia Katiba mpya,” alisema.

Rais Kikwete alivipongeza vyama hivyo vikubwa kwa kukubali kukutana kuzungumzia suala hilo na kwamba, wakati mazungumzo yanaendelea, ni vizuri kusiwapo na maneno maneno ya kuwachanganya viongozi wa vyama hivyo. “Natoa pongezi rasmi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Mtungi kwa kuvikutanisha vyama hivi.

Niwakumbushe kuwa wahenga walisema, miluzi mingi humpoteza mbwa... tusiseme seme maneno ya kuwachanganya badala yake tuwaombee... Bwana awape nguvu,” alisema Kikwete.

Alisema serikali pamoja na wananchi wana hamu kubwa ya kuona mchakato wa Katiba mpya unaendelea, hivyo ni fursa ya viongozi hao wa dini kuwaombea wajumbe hao wa Ukawa ili wapate wito na hatimaye kurudi bungeni kumalizia kazi iliyobaki

Aidha, Rais Kikwete alisema licha ya Tanzania kuwa na waumini wenye dini zenye madhehebu mengi, bado kuna changamoto kubwa ya kuongezeka kwa maovu.

Alisema kutokana na kuwapo kwa wingi wa madhehebu ya dini kunaashiria uwapo mkubwa wa waumini wanaomcha Mwenyezi Mungu na hivyo kupungua kwa maovu kwa kiasi kikubwa; jambo ambalo hata hivyo linaonekana kuwa kinyume.

“Tulitegemea kwa hali hii maovu mengi yangepungua sana katika jamii yetu. Lakini kinyume chake, maovu katika jamii yameongezeka sana na baadhi yake hufanywa na wale waliopewa dhamana ya kuchunga kondoo,” alisema. Rais Kikwete alisema yawezekana kuna mahali Watanzania wamekosea, hivyo makanisa hayana budi kutazama upya namna bora ya kuwaandaa vyema watu wake katika kuwalea ili kujenga jamii yenye hofu ya Mungu kwa kuwa na maadili mema.

“Nchini mwetu tumeshuhudia matukio ya kinyama ya mauaji kadhaa yakitokea, na mengine mengi ya ajabu yanatendeka kupitia miamvuli ya dini, kwa kweli matendo haya ni ya fedheha sana kwa nchi yetu na hayana budi kukemewa vikali,” alisisitiza.

Aliwataka viongozi wa dini zote nchini kudumisha ushirikiano na serikali katika kutatua changamoto zilizopo ndani ya jamii ili taifa liendelee kuwa na amani na utulivu.

AZINDUA KITABU
Rais Kikwete aliwatunuku baadhi ya wachungaji wa kanisa hilo nishani mbalimbali za utumishi kutokana na kazi nzuri walizozifanya za kijamii ndani na nje ya kanisa hilo pamoja na kuzindua kitabu kipya cha kanisa hilo kiitwacho 'Historia ya TAG'.

Awali, katika risala yake Askofu Mkuu wa TAG, Dk. Barnabas Mtokambali alisema kuwa kanisa hilo linakabiliwa na changamoto ya kupata usajili wa shule kutokana na masharti magumu yaliyowekwa na serikali ya kujenga majengo yote na vifaa ndipo wapewe usajili.

Alisema kanisa linasikitishwa na kinachoonekana kukwama kwa mchakato wa uundwaji wa katiba mpya hivyo kumwomba rais aingilie kati kuleta maridhiano mapema ili wajumbe wote waliotofautiana kuondoa tofauti zao kwa kuridhiana hivyo warudi  bungeni kutengeneza katiba kwa manufaa ya Watanzania.

SOURCE: NIPASHE

No comments:

Post a Comment