.

.

.

.

Monday

Papa Francis aruhusu wanamaombi kanisani

Papa amekuwa akisisitiza kuwa kuna umuhimu wa kanisa hilo kupambana na shetani na pepo.


Makao Makuu ya Kanisa Katoliki (Vatican), yametangaza kuwatambua rasmi makasisi wake wanaoombea na kutoa pepo wanaowashikilia waumini wao kama yanavyofanya makanisa ya Kipentekoste.

Uamuzi huo ambao ni wa kwanza kutolewa katika historia ya kanisa hilo, umetolewa juzi na Papa Francis na kuchapishwa kwenye gazeti la Vatican la L’Osservatore Romano.

Papa Francis (pichani) alibariki kundi la makasisi 250 kutoka nchi 30 ambalo huwaombea watu wenye pepo.

Alipoulizwa kuhusu uamuzi huo wa Papa, Makamu Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severine Niwemugizi, alisema taarifa hiyo siyo ya kushangaza kwa kuwa hata ndani ya kanisa ipo ibada ya kuombea wagonjwa.

Alisema ingawa hakuisoma taarifa hiyo, anaamini kwamba kwa kuwa kikundi hicho kimepewa idhini na Papa kinachotakiwa ni kufuata taratibu za kanisa.

“Kwa kuwa taarifa hiyo imetoka kwa Papa...tunafahamu ipo ibada rasmi ya kuombea pepo katika kanisa,” alisema Askofu Niwemugizi.

Iwapo tamko hilo la Papa likitekelezwa, waumini wanaweza kuanza kushuhudia baadhi ya makasisi wao wakiwaombea na kuwatoa pepo waumini kama inavyofanyika kwenye makanisa ya Kipentekosti.

Papa amekuwa akisisitiza kuwa kuna umuhimu wa kanisa hilo kupambana na shetani na pepo.

Mwaka jana alionekana akimwombea mtoto wa kiume kwa kumwekea mkono kichwani, tukio ambalo wanamaombi walisema alikuwa akimwombea aachiwe na ‘nguvu za giza.’

Katika hotuba yake ya kwanza, baada ya kuchaguliwa mwaka jana, Papa Francis alizungumzia suala la kupinga nguvu za pepo.

“Yeye ambaye haombi kwa Bwana anaomba kwa pepo. Wakati ambapo hatumtangazi Yesu Kristo, tunatangaza ulimwengu wa shetani, ulimwengu wa pepo,” alisema.

Kundi la kwanza la wanamaombi lilianzishwa na Padri Gabriele Amorth, miaka 30 iliyopita kwa kuwaombea watu mbalimbali wenye pepo ambao hupiga kelele wakati wakiombewa.

Mwaka 1991, Padri Amorth alianzisha kikundi cha maombi nchini Italia, baadaye alianza kuandaa mikutano mbalimbali ya kuwaombea watu wenye pepo katika nchi nyingine.

“Shetani hayupo kila mahali, lakini anapokuwapo husababisha maumivu,” alinukiliwa Amorth akisema mwaka 2010 wakati wa mahojiano.

Wakati huo, alisema kuwa alikuwa ameshawaombea watu 70,000 waliokuwa na pepo na kwamba akishirikiana na wenzake sita au saba alikuwa akiwakandamiza chini watu hao kwa kuwa shetani alikuwa akijibu mapigo.

“Shetani ni roho kabisa, isiyoonekana. Anaonekana wakati anapomtoka mtu kwa kupiga kelele. Anaweza kukaa kimya, akaongea lugha tofauti na hata kujibadilisha,” alisema.

Aliongeza kuwa baadhi ya watu aliokuwa akiwaombea walikuwa wakitapika vyuma vyenye ukubwa wa kidole cha mtu. Kufikia mwaka 2010 alikuwa amekwishahama ofisi 23 kutokana na kulaumiwa na makasisi wenzake kuwa watu anaowaombea wanapiga kelele.

Alisema matukio mawili ya Papa Yohane Paulo II kupigwa risasi na kujeruhiwa mwaka 1981 na pia Papa Benedict XVI kusukumwa wakati wa Krismasi mwaka 2009 kuwa yalikuwa matukio yaliyosababishwa na shetani.

“Naamini maaskofu wasiowateua wanamaombi wanafanya dhambi,” alisema.

Mkuu wa Wanamaombi, Francesco Bamonte, aliliambia L’Osservatore kuwa kutambuliwa kwa kundi hilo kumesababisha furaha kwa Kanisa lote, na kuongeza: “Wanamaombi ni mfumo wa kusaidia unaowapa faida wanaopata shida.”

No comments:

Post a Comment