.

.

.

.

Thursday

NIFANYE NINI BAADA YA KUSHINDWA VIBAYA, KUANGUKA VIBAYA NA KUMKOSEA MUNGU VIBAYA.

Hili neno limewaka kwa nguvu sana moyoni mwangu asubuhi hii ya leo baada ya kuamka na najua ni la mtu huko kwenye mitandao ya jamii.
Naomba baada ya kulisoma lisukume mbele kwa wengine maana huwezi kujua ni watu wangapi wanaweza kusaidiwa na huu ujumbe toka kwa Bwana.
Nazungumza na mtu ambaye anajihisi ameshindwa vibaya sana, ameanguka vibaya na amemkosea Mungu vibaya sana.
Unajisikia vibaya na unahisi kama mzigo mzito sana wa huzuni, majonzi,hatia, majuto upo katika moyo wako.
Kwanza nikuambie kuwa haupo pekee yako.
Kila mmoja wetu katika maisha yake huwa anafikaga mahali kama hapo baada ya kufanya jambo ambalo linamfanya ahisi kuwa ameshindwa vibaya sana, ameanguka vibaya na amemkosea Mungu vibaya mno.
Ni hali ngumu sana kujisikia hivyo na ni hali inayotesa mno.
Binafsi ninachoenda kuandika humu sio nadharia bali ni mambo ambayo nimeona yakifanya kazi katika maisha yangu mwenyewe binafsi na najua yatafanya kazi kwako pia.
Nataka tuanze kuangalia maandiko ambayo najua yatatusaidia sana.
Luka 22: 31, 32.
31 Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; 32 lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.
Kabla Petro hajaingia katika hali kama hii ambayo nimeitaja kwenye hili somo, alionywa na Bwana Yesu pamoja na wenzake kuwa shetani amewataka apate kuwapepeta kama ngano na hayo alikuwa anayasemea kwa habari ya mambo ambayo yataenda kutokea kipindi kifupi kijacho wakati Yesu atakapokamatwa na kuwekwa mikononi mwa wabaya ili kuteswa.
Anamwambia Petro kuwa amemwombea yeye ili imani yake isitindike.
Mara nyingi mtu unapohisi umeshindwa vibaya, umeanguka vibaya na umekosea vibaya, unashuka moyo kiasi kwamba imani inaweza ikatindika au ukatindikiwa na imani.
Unajiona hufai tena.
Unajiona hutoshi tena kwa ajili ya Bwana.
Unajiona hustahili kwa ajili ya utumishi tena.
Yesu alilijua hili na aliliona hili linakuja na akamwombea hasa Simoni maana hili jambo lingemwathiri Petro kuliko mwanafunzi mwingine yeyote.
Yesu alimwombea imani yake isitindike na akamwambia atakapoongoka basi awasaidie na wenzake.
Kuongoka ni kubadilika toka kwenye hiyo hali ya kushindwa, kuanguka au kumkosea Mungu vibaya sana na kumrudia Mungu na rehema Zake, huruma Zake, fadhili Zake, neema Zake na msamaha Wake.
Haijalishi umeshindwa kiasi gani, umeanguka kiasi gani na umemkosea Mungu kiasi gani unaweza kugeuka.
Unaweza kubadilika.
Unaweza kutengeneza na Mungu ukarejea.
Hali kama hizi zinaweza kukunyenyekeza sana.
Unyeyekevu ni jambo jema sana.
Inakuweka kwenye nafasi ya kuweza kusaidia wengine baadaye.
Maandiko yanasema:
Waebrania 5: 1, 2.
1Maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi; 2 awezaye kuwachukulia kwa upole wao wasiojua na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu;
Kuhani Mkuu alikuwa ni mwanadamu, amewekwa kwa ajili ya wanadamu wengine katika mambo yamhusuyo Mungu ilia atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi.
Kila mmoja wetu aliyeokoka ni kuhani na ana huduma hiyo hiyo ya kwenda mbele za Mungu kufanya maombi, dua, sala, maombezi kwa ajili ya wengine kwa ajili ya dhambi na makosa ambayo wao wanafanya.
Moja ya vitu ambavyo kuhani yeyote anatakiwa kuwa nacho ni uwezo wa kuchukuliana kwa upole na wale wanaokosea.
Kinachoachilia huo uwezo ndani yake ni pale ambapo yeye mwenyewe anapokutana na mambo yayo hayo na Mungu anamsaidia kumtoa.
Ndo maana Yesu alimwombea kipekee Petro na akamwambia atakapoongoka awasaidie ndugu zake.
Mungu anakutoa ili na wewe uwatoe wengine.
Siku moja Yesu akiwa anazungumza na wanafunzi wake aliwaambia:
Mathayo 10: 32, 33.
32Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. 33 Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
Petro alikuwepo naye wakati Yesu anazungumza maneno haya.
Sasa unaweza kujua kilichokuwa kinaendelea ndani ya Petro wakati Yesu aliposema naye maneno yanayofanana na hayo siku za usoni.
Luka 22:33, 34.
33Akamwambia, Bwana, niwapo pamoja nawe, mimi ni tayari kwenda gerezani au hata kifoni. 34Akasema, Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla wewe hujanikana mara tatu ya kuwa hunijui.
Yesu alipotoka tu kumwambia Petro jinsi ambavyo shetani amewataka ili awapepete kama ngano na kwamba amemwombea yeye Petro ili imani yake isitindike na kwamba akiongoka awasaidie na wenzake, Petro kwa kiherehere chake kama kawaida akajibu akasema yupo tayari kwenda gerezani au hata kufa kwa ajili ya Yesu.
Kwa maneno mengine alikuwa anajaribu kumwambia Yesu kuwa wote watamkimbia ila yeye hatamkimbia.
Petro alikuwa amejaa kiburi cha uzima.
Maandiko yanasema:
I Kor 10: 12
12Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.
Petro alikuwa anajiamini kupita kiasi na alijiona yeye hawezi kumwangusha Yesu kama hao wengine.
Yesu ilikuwa kama anamwambia Petro, hawa wenzako watakimbia na kuniacha, wewe utabaki, ila utanikana.
Afadhali hawa wamekimbia.
Ila wewe utanikana.
Nafikiri Petro aliwaza uzito wa kosa hilo la kumkana Yesu mbele za watu maana Yesu alishasema mtu akimkana mbele za watu, Yeye atamkana mbele za Baba Yake aliye mbinguni.
Petro akaona kama vile Yesu hajui anachoongea.
Petro alikuwa anakaribia kushindwa sana, kuanguka sana na kumkosea Yesu sana.
Yesu aliliona hilo linakuja akamwombea.
Kama Yesu alivyomwambia Petro ndivyo ilivyoenda kutokea.
Luka 22: 54 – 62.
54 Wakamkamata, wakamchukua, wakaenda naye nyumbani kwa Kuhani Mkuu. Na Petro alimfuata kwa mbali. 55Na walipokwisha washa moto katikati ya kiwanja, waliketi pamoja, naye Petro akaketi kati yao. 56Ndipo mjakazi mmoja akamwona ameketi mwangani, akamkazia macho akasema, Na huyu alikuwa pamoja naye. 57Akakana, akisema, Ee mwanamke, simjui. 58Baadaye kitambo mtu mwingine alimwona akasema, Wewe nawe u mmoja wao. Petro akasema, Ee mtu, si mimi. 59Halafu, yapata saa moja, mtu mwingine alikaza kusema, Hakika na huyu alikuwa pamoja naye, kwa kuwa yeye pia ni Mgalilaya. 60Petro akasema, Ee mtu, sijui usemalo. Na papo hapo alipokuwa katika kusema, jogoo aliwika. 61 Bwana akageuka akamtazama Petro. Petro akalikumbuka lile neno la Bwana jinsi alivyomwambia, Leo kabla hajawika jogoo utanikana mara tatu. 62Akatoka nje akalia kwa majonzi.
Kile kile ambacho Petro alidhani hawezi kamwe kufanya alikifanya tena si mara moja wala mara mbili bali mara tatu kwa usiku moja.
Hakika Petro alishindwa vibaya, alianguka vibaya na kumkosea Mungu vibaya sana.
Alafu mbaya zaidi alipomkana Yesu mara tatu alafu jogoo akawika, Yesu akageuka kumwangalia Petro na macho yao yalipokutana, ni kama Yesu alikuwa anamwambia Petro, Unaona? Nilikuambia nini?
Petro akakumbuka alichoambiwa na Bwana, akatoka nje akalia kwa majonzi sana.
Petro alilia kwa sabahu ya uzito wa kosa ambalo alikuwa ametoka kulifanya.
Amemkana Yesu sio mara moja, bali mara tatu.
Lazima aliwaza, huu mchezo ndo ushakwisha.
Yesu Naye atanikana mbele za Baba Yake.
Alikuwa katika hali ngumu sana na hiyo hali hatujui iliendelea kwa muda gani ila tunachojua ilimwathiri mnooooooo.
Ukitaka kujua ilimwathiri kiasi gani, embu angalia haya maneno yafuatayo:
Marko 16: 6, 7.
6Naye akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka. 7 Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia.
Malaika alipotuma ujumbe kupitia wale wanawake watatu ambao walienda kaburini kwa wanafunzi wa Yesu, aliwaagiza wale wanawake waende kwa Petro pia wakamwambie hayo maneno maana wangesema Yesu atakutana na wanafunzi, Petro asingeenda maana kwa kosa lake tayari ameshakanwa Naye.
Mungu aliye mwingi wa rehema alimpa Petro nafasi nyingine pamoja na ukubwa wa kushindwa kwake, anguko lake na kosa lake.
Ninaamini hata kama umeshindwa kiasi gani, umeanguka kiasi gani na kukosea kiasi gani bado Mungu anayo nafasi nyingine kwa ajili yako.
Kinachohitajika kutoka kwako ni unyenyekevu na kukubali kuwa umekosea.
Tunajua Yesu alipokutana na wanafunzi pamoja na Petro ilibidi maalumu amrejeshe Petro kwa kumwuliza mara tatu kama kweli anampenda ili kufuta vile alivyomkana mara tatu.
Yohana 21: 15 – 17.
15 Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu. 16 Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. 17 Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.
Hata wewe unaweza kurejezwa.
Nyenyekea urejezwe na Bwana.
Wapo watu wengi wamemziria Yesu katika huduma kwa sababu ya kushindwa kwao, kuanguka kwao na kumkosea Mungu kwao.
Wanajiona wapo sahihi lakini kimsingi ni kiburi ndo kinawatesa.
Na hicho kiburi na majivuno ndo kinawaathiri zaidi kuliko kushindwa kwao, anguko lao na kukosea kwao.
Inahitaji unyeyekevu wa hali ya juu sana kuweza kumtumikia tena Mungu baada ya kushindwa, kuanguka na kumkosea Mungu.
Wengi wanajihukumu na hawajui kwa kufanya hivyo wanajifanya Mungu.
Petro rudi kwenye utumishi ili ukasaidie wengine ambao wanashindwa, kuanguka na kumkosea Mungu kama wewe maana kwa mtu ambaye hajawahi kupita hapo hawezi kujua jinsi ya kumsaidia mwingine.
Sana sana atamhukumu tu.
Rudi kwenye utumishi Petro.
Kukataa kumtumikia Mungu ni udhihirisho ni kwa kiasi gani humpendi Mungu na ndo maana Yesu alitaka kujua kutoka kwa Petro kama kweli anampenda.
Yamkini kupitia somo hili Yesu anakuuliza kama kweli unampenda.
Usijibu ndiyo ali hali haupo tayari kumtumikia katika eneo la vipawa, karama na huduma ambazo amewekeza ndani yako.
Unaweza kuniambia, Carlos nitawezaje kufanya hivyo?
Kumbuka tu:
Warumi 11: 29.
29Kwa sababu karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake.
Daudi alimkosea Mungu vibaya sana lakini katika toba yake alimwomba Mungu kwa kusema:
Zaburi 51: 13.
13Nitawafundisha wakosaji njia zako,
Na wenye dhambi watarejea kwako.
Daudi aliujua moyo wa Mungu na alijua kuwa pamoja na kwamba ameshindwa vibaya, na kuanguka vibaya na kumkosea Mungu vibaya sana lakini bado angeweza kutumika na Mungu kuwafundisha wakosaji njia za kumrejea Mungu ili warejee kwa Mungu kama ambavyo yeye karejezwa kwa Mungu.
Kuna kitu natamani ukione kwa Daudi.
Pamoja na kushindwa kwake, kuanguka kwake na kukosea kwake, Daudi alikuwa mnyenyekevu na mwenye moyo uliyopondeka.
Zaburi 51: 17.
17Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika;
Moyo uliovunjika na kupondeka,
Ee Mungu, hutaudharau.
Vunjika na kupondeka mbele za Mungu.
Rejea kwenye safu huku ukiwa mnyenyekevu zaidi na huku ukijua kuwa unamhitaji sana Mungu ili kuweza kusimama na kutoshindwa, kuanguka na kumkosea.
Hiyo hali ya kuendelea kukaa pembeni ni kiburi na majivuno.
Mungu anataka nini kwako:
Mika 6: 8.
8Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na BWANA anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!
Rejea kwenye safu, tenda haki lakini muhimu sana penda rehema sio kuwahukumu hukumu wengine.
Usije ukasahau jinsi ulivyoshindwa, anguka na kumkosea Mungu alafu Mungu akakurejesha.
Acha kuhukumu wengine wakati na wewe ni mfaidika wa rehema za Mungu.
Waongoze wengine kwenye rehema za Mungu zitakazo warejesha kama wewe ulivyo rejeshwa.
Na bila kusahau sasa enenda kwa unyenyekevu mbele za Mungu wako huku ukijiangalia sana kwa msaada wa Mungu wewe mwenyewe usije shindwa tena, anguka tena na kukosea tena.
Unaweza kuniambia, Mchungaji nahisi Mungu yupo mbali sana.
Kama kweli unahisi hivyo, basi tatizo sio kushindwa kwako, wala anguko lako wala kosa lako.
Una majanga na maswala ya unyenyekevu.
Maandiko yanasema:
Zaburi 34: 18.
18BWANA yu karibu nao waliovunjika moyo,
Na waliopondeka roho huwaokoa.
Kama humhisi karibu nawe basi tatizo umepoteza hali ya kuvunjika na kupondeka mbele Zake.
Mtu wa Mungu, vunjika na kupondeka mbele Zake.
Nimalize na hili andiko:
Isaya 57: 15.
15 Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu.
Aise embu rudi kwenye utumishi.
Unazidi kuharibu sasa kuliko ulivyoharibu kupitia kushindwa kwako, kuanguka kwako na kukosea kwako.
Naamini kuna mtu amesaidika sana na ujumbe huu wa leo.
Tafadhali share huu ujumbe kwa kadiri iwezekanavyo maana hujui ni nani utamsaidia.
Mungu akubariki sana.

MCHUNGAJI NA MWALIMU
CARLOS RICKY WILSON KIRIMBAI.
WHATSAPP#: +255786312131.

No comments:

Post a Comment