.

.

.

.

Monday

Waziri Mkuu Majaliwa akabidhi utumbuaji majipu kwa maaskofu.

Viongozi wa dini nchini wametakiwa kuendelea kuiombea serikali ya awamu ya tano ili iendeleze kazi ya kutumbua majipu ambayo inagusa baadhi ya watu wenye nguvu serikalini.
 
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri Mkuu Kassimu Mjaliwa,  alipokuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za kumsimika Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelist Assemblis Of God Tanzania (EAGT) Dk. Brown Mwakipesile.
 
Majaliwa alisema ni muhimu kuiombea serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli ambayo imekuwa ikisimamia uwajibikaji kwa kuwa utumbuaji majipu unahitaji maombi zaidi kutokana na kuwa na vikwazo vingi.
 
“Watu hawapendi kuguswa maslahi yao, mtuombee kazi ya kutumbua majipu ni ngumu. Serikali itafanya kazi kwa kufuata sheria na taratibu na haitamwonea mtu,” alisema.
 
Alisema kama kuna mtumishi ambaye anaona haendani na kasi ya utendaji kazi awamu ya tano, apishe kwa kuwa kuna wasomi wengi wanaohitaji ajira. 
 
Pia alisema ili kuendelea kutoa huduma nzuri lazima mapato ya serikali yanayokusanywa yasimamiwe na kukusanywa kwa ufasaha. Alisema anajua kuna kundi litakasirika kutokana na utendaji kazi wao.
 
“Wanaosema hii ni nguvu ya soda wanajidanganya, kwani tumedhamiria na jitihada zetu ni kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa zinarudi kwa ajili ya kusaidia wananchi,” alisema.
 
Aidha alisema kuwa serikali inaanza kupitia maeneo yote muhimu yatakayofanya Watanzania kupata huduma kwa ukamilifu na moja ya maeneo yatakayoangaliwa katika bajeti ijayo ni kupunguzwa kwa vifaa vya gharama ya ujenzi.
 
Alisema kuna baadhi ya taasisi za dini zinazotumia vibaya nafasi za kuingiza bidhaa bila ushuru na kuwanyima fursa wale wenye malengo mazuri wanaotaka kuifanya kazi ya Mungu kwa uwazi na ukweli.
 
Waziri Mkuu pia alisema atakuwa na kikao na viongozi wa dini zote ili kujadili mambo yanayotakiwa kufanywa kati yao na serikali ili kuwa kitu kimoja.
 
Kuhusu mpango wa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, alisema serikali ilitenga Sh. bilioni 131.6 kuhudumia shule hizo kuanzia Januari hadi Juni, mwaka huu.
 
Alisema wameanza na changamoto nyingi lakini wataendelea kuboresha kutokana na serikali kuwa na mpango mzuri kwenye jambo hilo.  Pia alisema ubora wa elimu utaendelea kuimartishwa.
 
Naye Askofu Mkuu Mwakipesile alisema kanisa hilo lina malengo ya aina mbili ambayo ni ya kiroho na kimwili.
 
Alisema kwa sasa Kanisa hilo lina jumla ya makanisa 5,000 Tanzania nzima huku wakiwa na zaidi ya majimbo 90 na Kanda tisa.
 
Dk. Mwakipesile aliahidi kuwa kanisa hilo litaendelea kuombea nchi ili iwe na utulivu, amani na  mshikamano.
 
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa EAGT, Leonard Mwizarubi, alisema kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu inaleta hamasa kubwa kwa kanisa kwa kuwa wanaaminmi uchumi utaimarika.
 
Askofu Dk. Mwakipesile anakuwa Askofu Mkuu wa pili wa kanisa hilo baada wa Askofu Mkuu wa Kwanza, Dk. Moses Kulola, kufariki dunia  Agosti 29, 2013.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment