.

.

.

.

Tuesday

NEC yatoa mwongozo utangazaji matokeo

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imetoa hadharani mfano wa karatasi  zitakazotumika kupigia kura kwa ajili ya kumchagua Rais wa awamu ya tano wa Tanzania Oktoba 25, mwaka huu.
 
Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari Nec,  Clarence Nanyaro , alisema karatasi hizo zimegawanywa katika makundi mawili.
 
Alisema kundi la kwanza ni wapiga kura wasio na ulemavu wa aina yeyote na nyingie ni kwa ajili ya wapiga kura wenye ulemavu.
 
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva.
“Huu ndiyo mfano wa karatasi za kupigia kura za watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu ambazo zitawekwa kwenye kisanduku cha wazi baada ya kuweka alama ya tiki,” alisema huku akionyesha fomu hizo.
 
MATOKEO YA URAIS YATAKAPOTANGAZWA
Nanyaro alisema matokeo ya kura za urais yatatangazwa katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
 
Alisema tayari ukumbi huo umeanza kutengenezwa ili kuwekwa katika mazingira mazuri zaidi kwa ajili ya tukio hilo la kihistoria.
 
Alisema kati ya maeneo yanayotengenezwa ni pamoja na eneo ambalo litakuwa maalum kwa waandishi wa habari pamoja na sehemu ya kupokelea matokeo hayo.
 
Nanyaro alisema  matokeo ya kura za urais yatakuwa yanapokelewa kwa mfumo wa kielekroniki kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na kujumlishwa kabla ya mshindi kutangazwa rasmi.
 
SIKU YA MATOKEO KUTANGAZWA
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imefichua siku itakayomtangaza rasmi mshindi wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni Oktoba 28, mwaka huu.
 
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mkutano na wawakilishi wa walemavu na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, alisema watamtangaza mshindi wa nafasi hiyo baada ya siku tatu kuanzia siku ya kupiga kura (Oktoba 25, mwaka huu) kwa sababu watakuwa wameshakamilisha kazi ya kupokea na kujumlisha kura zote kutoka katika mikoa yote nchini.
 
Jaji Lubuva alieleza zaidi kuwa wamejiandaa vya kutosha na hivyo wana uhakika wa kutangaza matokeo hayo ndani ya siku tatu tofauti na ilivyokuwa katika chaguzi kadhaa zilizopita.
 
MFUMO UTAKAOTUMIKA
Akifafanua zaidi kuhusiana na suala hilo wakati akiwasilisha mada mojawapo katika mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Nec, Emannuel Kawishe, alisema mfumo wa kujumlisha matokeo utakaotumika mwaka huu (Result Management System) ndiyo unaowapa uhakika zaidi wa kukamilisha malengo yao kwani wenyewe ni maalumu kwa kuondoa makosa mbalimbali ya kibinadamu yanayoweza kutokea katika ujumlishaji wa kura.
 
“Mfumo huu siyo mgeni kwani ulitumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na 2010, changamoto zilizojitokeza uchaguzi uliopita hazitajirudia,” alisema na kuongeza:
 
“Tume imeandaa mfumo mbadala wa ‘Spreadsheet Excel RMS ambao utatumika iwapo kutakuwa na changamoto katika kutumia mfumo ulioandaliwa.”
 
Kawishe alikiri kuwa utumaji wa matokeo ulikuwa na changamoto nyingi katika uchaguzi wa 2010 kwani kati ya majimbo 239 ni majimbo 150 ndiyo yaliyoweza kutuma matokeo kwa mfumo uliokuwa umeandaliwa wa simu za mikononi na nukushi (fax).
 
“Hivi sasa Tume inafanya maandalizi ya kutumia Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa, kutuma matokeo yote badala ya kutumia mtandao wa simu za mkononi. Itasaidia upatikanaji wa matokeo mapema kama inavyokusudiwa na njia mbadala ya fax imeandaliwa na halmashauri zote zimepewa vifaa vitakavyowezesha utumaji wa matokeo kwa haraka,” alisema.
 
Kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343, kifungu 81 cha Sheria ya Uchaguzi wa Mitaa, sura ya 292, Nec ndiyo yenye mamlaka kisheria kujumlisha na kutangaza matokeo ya uchaguzi wa Rais.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment