.

.

.

.

Monday

Kardinali Pengo atofautiana na Maaskofu


Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo akibariki matoleo yakiotolewa na Umoja wa Wanawake wa katoriki(WAWATA), wakati wa Ibada iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis 

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema waumini hawana budi kusoma vizuri na kuelewa Katiba Inayopendekezwa ili wakati ukifika, wafanbye uamuzi kwa hiari na utashi wao wakati wa kupiga Kura ya Maoni.

Ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku mbili baada ya Jukwaa la Wakristo kutoa tamko linalowataka waumini kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura, kushiriki kikamilifu kwenye shughuli zote za elimu ya Katiba Inayopendekezwa na kupiga kura ya “hapana” kuikataa Katiba Inayopendekezwa.

Lakini jana, Kardinali Pengo alisema kuisoma na kuielewa katiba hiyo ndiyo wajibu wa msingi ambao Wakristo wanao kwa sasa ili kupiga kura inayostahili wakati ukifika. Kuhusu maaskofu kuagiza waumini waikatae Katiba Inayopendekezwa, Kardinali Pengo alisema wao wakiwa viongozi wa watu, hawana mamlaka wala uwezo huo, bali wenye uwezo ni wananchi wenyewe.

Hata hivyo, Kardinali Pengo alitaka tamko hilo lisambazwe kwenye parokia na vigango vyote vya Jimbo Kuu la Dar es Salaam ili waumini wasomewe, wauelewe kwanza, ili hatimaye waweze kufanya uamuzi sahihi wakielewa ni nini wanachokitakiwa kukifanya.

Changamoto za familia

Katika hatua nyingine, Kardinali Pengo pia alizungumzia changamoto za wanandoa, ikiwamo tabia ya kuchepukia nje ya ndoa ambayo alisema inasababisha amani kutoweka ndani ya familia.

Akizungumza katika ibada ya Kwaresima kwa Wanawake Wakatoliki Tanzania (Wawata) jana, Kardinali Pengo alisema akina mama wengi kwa sasa, hususan katika ndoa wamekuwa wakisaliti ndoa na baadaye kuwatupia lawama watoto wao juu ya tabia walizoanzisha wenyewe.

Katika mahubiri yake aliyoyatoa katika Kanisa la Mt. Joseph Dar es Salaam, mbali na changamoto sugu za kifamilia, Kardinali Pengo alijikita katika kuangalia aina sita za malezi kwa watoto na athari za utandawazi kwenye jamii.

“Wapo wanawake ambao kwa sasa wanaendekeza michepuko kwenye familia na wamekuwa hawana hofu ya Mungu wakati wote. Kuna wengine ambao wanavaa mavazi ya mabinti wakisema wanakwenda na wakati,” alisema.

“Wanawakemea watoto wao wakati wao wanaendekeza tabia chafu, wakiulizwa wanasema eti wao wameshakuwa watu wazima.”

Katika sehemu ya mafundisho yake, mbali na kupungua uaminifu, Kardinali Pengo alizitaja changamoto nyingine alizosema kuwa zimeendelea kuumiza familia ambazo ni tofauti za kiimani, kipato, elimu, kulea watoto nje ya ndoa, kushindwa kudhibiti maadili ya watoto, ushirikina na ufisadi.

Alisema changamoto hizo zinatafuna familia nyingi kwa sasa.”Familia inayokuwa inaendeshwa kwa imani tofauti za kidini ni changamoto kubwa sana, amani inapungua ndani ya familia kwa hivyo tunahitaji kuwa makini na changamoto hizo,” alisema Kardinali Pengo.


Source:mwananchi

No comments:

Post a Comment