.

.

.

.

Friday

Askofu Nzigilwa afunguka kuhusu fedha za Rugemalira

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Eusebius Nzigilwa.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Eusebius Nzigilwa, amesema atatoa ufafanuzi wa  shutuma zinazomkabili za kuingiziwa fedha katika akaunti yake kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa VIP Engeneering& Marketing LTD, James Rugemalira, baada ya  Bunge kujadili ripoti ya uchunguzi wa uchotaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya Tegeta Esrcow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Askofu Nzingilwa alikiambia chanzo jana kuwa anachosubiri kwa sasa ni majadiliano yaliyokuwa yakiendelea jana bungeni kuhusu sakata hilo yamalizike ndipo atoe ufafanuzi kuhusiana na yeye kuhusishwa kwenye mgawo wa fedha hizo.

Alisema anashangaa kutajwa katika ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwa alipokea Sh. milioni 40 kutoka  Rugemalira bila kuitwa na kuhojiwa.

Askofu  Nzigilwa, alisema  hakuwahi kupigiwa simu wala kuitwa kuhojiwa  juu ya fedha hizo, hivyo atakutana na vyombo vya habari na kulitolea ufafanuzi.

“Nimeshindwa kuelewa kuhusu jambo hili, kwani mpaka maoni ya ripoti hiyo yanawasilishwa bungeni juzi, sikuwahi kuhojiwa nao kuhusu fedha nilizoingiziwa  kwenye akaunti yangu,” alisema Askofu Nzigilwa.

Alisema kuwa alimfahamu Rugemalira kipindi alipokuwa Paroko wa Parokia ya Makongo Juu, Dar es Salaam  kwa hiyo ni mtu wake wa karibu na haoni hatari kuingiziwa fedha hizo na mtu anayemfahamu.

Aliongeza kuwa  ripoti iliyowasilishwa bungeni  na kumtaja, haikufafanua  ushiriki wake katika sakata hilo zaidi ya kueleza kuingiziwa fedha kwenye akaunti yake kupitia Benki ya Mkombozi . Alisema yeye ni mteja wa kawaida na hayuko katika kamati yoyote ama nafasi yoyote ya uongozi katika benki hiyo.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment