.

.

.

.

Monday

Maaskofu Wakatoliki wamtwisha zigo Rais Kikwete


Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limeshangazwa kuzuka kwa mabishano makali na mpasuko uliosababisha upotoshaji wa nia iliyokusudiwa katika Bunge Maalum la Katiba baada ya hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ya kulizindua Februari 18, mwaka huu.

 Kauli ya TEC ilitolewa jana mjini hapa na Rais wake, Askofu Tarcius Ngalekumtwa, alipozungumza na waandishi wa habari kwa lengo la kutoa tamko hilo.

“Tukumbuke Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uthubutu na ujasiri wa kipekee alianzisha mchakato wa kuunda katiba mpya, na kisha aliridhia kwa kuipokea rasimu ya pili kwa furaha rasimu ya pili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema na kuongeza:

Rais Jakaya Kikwete

“Ni lazima sasa tujiulize, nini kimetokea hadi kugeuka kabisa mwelekeo mzima  wa mabadiliko ya Katiba kwa kuikejeli na kuishutumu vikali rasimu hiyo katika wakati wa kipekee kabisa wa kihistoria wa uzinduzi wa Bunge Maalum la Katiba. Hata kusahau gharama kubwa ambayo ilibebwa na walipa kodi, na sasa hali inaonyesha dhahiri jambo hili limeiingiza nchi katika mgogoro mkubwa unaoashiria hatari mbeleni.”

Ingawa tamko hilo halikufafanua kilichotokea wakati wa uzinduzi, lakini Rais Kikwete aliweka wazi msimamo wake kwamba rasimu ya pili ya Katiba ilikuwa na kasoro nyingi na kusema kwamba wajumbe wa Bunge hilo wanapaswa kusoma ukurasa kwa ukurasa, sentensi kwa sentensi, neno kwa neno na wakiona kuna mambo ya kubadilisha wayabadilishe.

Baadhi ya mambo ambayo Rais alisema Tume hiyo iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba ni muundo wa serikali akisema kwamba muundo wa serikali tatu uliopendekezwa haufai kwa kuwa hauwezi kudumisha muungano na kwamba serikali mbili zilizofanyiwa marekebisho ndizo zitakazoudumisha.

Ngalekumtwa alisema maoni ya TEC ni kuwa tatizo hilo kubwa ambalo limekuwa kikwazo kikubwa linaonyesha kukosekana utashi wa kisiasa na wahusika kutokuwa wakweli juu ya suala zima la mchakato wa Katiba.

 TEC wamewataka wajumbe wa  Bunge Maalum la Katiba kuwa wamoja na kufanya kazi yao kwa mtazamo usiotegemea siasa za vyama kwa lengo la kunusuru mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya.

“Kuandika katiba ni kazi iliyo ngazi ya juu zaidi ya siasa za vyama, hivyo utashi wa kisiasa wa kuunda Katiba mpya kwa kuzingatia rasimu ya pili utaweza kuridhiwa kwa kuzingatia msingi huu,” alisema Rais huyo ambaye pia ni Askofu wa Jimbo la Iringa.

 Aliongeza: “Kwa hiyo tunawasihi kwa mara nyingine tena ninyi wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kurejea katika sehemu ya pili ya mjadala Agosti mkiwa na moyo na mtazamo mpya. Tunawaomba achaneni kabisa na ubinafsi, uwe wa mtu mmoja, ama katika vikundi.”

 Kwa kazi yenu tusaidieni sisi Watanzania tuweze kujivunia kuwa na Taifa adilifu tukifanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya manufaa na ustawi wa wote .

Kumbe Bunge Maalum la katiba mnao wajibu wa kimaadili kwa nchi yenu na vile vile kwa namna mnavyotekeleza wajibu wenu mnaandika historia ya nchi yenu.” Ngalekumtwa alisema kuwa kwa kadri ya nchi ilivyo  ziko sababu za kutosha za kutaka Katiba mpya. Alizitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na ufisadi, wananchi kujisikia kukosa usalama, nchi kutokuwa na dira , tunu msingi nakadhalika.

Alisema Katiba ya sasa ya mwaka 1977 ina upungufu unaopelekea kuendelea kuleta migogoro mikubwa yenye kuhatarisha amani nchini.

 Ngalalekumtwa alisema wakati huu Watanzania kwa pamoja wanatakiwa kuungana na kuwakumbusha wale wote  waliopewa dhamana ya kukamilisha rasimu ya pili ya  Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuwajibika binafsi na katika maridhiano ili waweze kupata katiba bora.

“Katika siku 67 ninyi wateule wa Rais mpatao 600 mkijadiliane pasipo umoja, mkishambuliana kwa kauli kali kati yenu, mkikashifiana pasipo udhibiti wa uongozi mliojichagulia wenyewe kwa kanuni na sheria mlizojitungia, mwenendo huu ni wa kusikitisha na kuchukiza katika jamii na mahali pale panapoheshimiwa na watu wote (bungeni),” alisema na kuendelea:

"Wajibu mliokabidhiwa ikiwa mtautekeleza kwa dhamira njema, mtalijengea taifa letu msingi imara, uliosheheni tunu za kimaaadili ambazo ni heshima katika utu wa mwanadamu, umoja na mshikamano na kujali manufaa ya taifa.”

Alisema matunda ya kazi ya wajumbe hao yawe ni ya kulipatia taifa dira inayowapa watu msukumo wa kujenga  taifa pamoja na  watu wamoja na wanaojadiliana kwa staha.

Aliongeza kuwa ikiwa matokeo yatakuwa yenye kuleta mema na kuimarisha amani na utulivu nchini watu wote watawashukuru na kuwasifu, lakini kama tunda la kazi yao litakuwa la kuingiza nchi kwenye matatizo zaidi, kuwataabisha wananchi na kukosa maelewano baina yao basi watu watawahukumu na kuwawajibisha kwa kukosa umakini katika jukumu walilokabidhiwa.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment