.

.

.

.

Monday

Padri awataka waandishi kuthamini utu

Waandishi wa habari wameaswa kujali utu wa mtu katika utekelezaji wa majukumu yao, pasipo kuathiri misingi na maadili ya tasnia hiyo.

Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Joseph Massenge, ameyasema hayo wakati akizungumza na wanachama wa Umoja wa Wanawamawasiliano jimboni humo (Umakada).

Mkutano wa wanamawasiliano hao, ulifanyika jana kwenye kituo cha Msimbazi jijini Dar es Salaam, kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki.

Padri Massenge, alisema hivi sasa tasnia ya habari inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo kama waandishi wa habari hawatatilia mkazo umuhimu wa kutambua na kuthamini utu wa mwanadamu, ipo hatari ya kuchochea chuki miongoni mwa watu.

Kwa mujibu wa Padri Massenge, miongoni mwa mambo yanayochangia kuwashawishi baadhi ya waandishi kujikuta katika hatari ya kutothamini ama kutambua utu wa mwanadamu ni hongo.

“Unapokubali kupokea bahasha (hongo) ili umchafue mtu fulani pasipo kujali ama kutambua thamani yake kwa jamii, unakuwa umechangia kusababisha chuki kwenye jamii,” alisema.

Akizungumzia kuhusu Umakada, Padri Massenge, alisema Umoja huo unapaswa kuwaunganisha Wanamawasiliano Wakatoliki, ukilenga kuwaibua na kuwaendeleza vijana wenye vipaji ama taaluma za uandishi wa habari na mawasiliano ya jamii.

“Mtakapojitoa na kufanikisha azma ya kuwaibua na kuwaendeleza mawasiliano ya vijana, mtakuwa mnatenda mambo mema…na hizo ndizo fadhila mbele ya Mwenyezi Mungu,” alisema.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment