.

.

.

.

Tuesday

Moravian siyo ulingo wa siasa - Mwaiseje

Mwenyekiti wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Misheni ya Mashariki, Mchungaji Samwel Mwaiseje, amesema ataendelea kuchukua hatua za kuyavunja mabaraza ya wazee wa sharika kulingana na tamko la sinodi.

Mchungaji Mwaiseje amesema kanisa hilo haliwezi kukubali kugeuzwa ulingo wa siasa na baadhi ya watu wanapuuza miongozo na maelekezo ya viongozi halali ya kanisa hilo kwa maslahi yao binafsi.

Amesema kwamba chini ya utaratibu huo, uongozi umebaini kuwapo kwa watu katika mabaraza hayo ya wazee, wanaoshinikiza waumini kukaidi maelekezo ya msingi yanayotolewa na viongozi wa ngazi za juu kwa maslahi yao binafsi.

Akizungumza na waumini wa kanisa hilo Usharika wa Kinondoni, Mchungaji Mwaiseje, alisema pamoja na kuibuka kwa makundi ya waumini wachache wanaompinga, lakini ukweli ni kwamba yeye ndiye Mwenyekiti halali wa jimbo hilo.

Mchungaji Mwaiseje alisema inasikitisha kuona wachungaji na baadhi ya viongozi wa mabaraza la wazee wakiongoza kwa utovu wa nidhamu na kukaidi maagizo muhimu yaliyotokana na mkutano mkuu wa kanisa (Sinodi) uliofanyika mkoani Morogoro na kusimamiwa na Askofu Dk. Lusekelo Mwakafwila.

Mchungaji Mwaiseje aliongeza kuwa pamoja na mambo mengine, mkutano huo uliokuwa na baraka za Unity Board, ulivunja uongozi wa zamani na kumchagua yeye kuwa Mwenyekiti na Mchungaji Saul Kajula, kuwa Makamu Mwenyekiti.

Aidha, mkutano huo ulimchagua Adolf Mwakanyamale, kuwa Katibu Mkuu, wachungaji watatu Owden Ndile, Allan Kajuni na Aswile Mwamkumbi, kuwa wenyeviti wa wilaya za Dar es Salaam (Kusini), Dar es Salaam (Kaskazi) na Morogoro ambao kikatiba watafanya kazi chini ya Mwenyekiti Mwaiseje.

“Mkutano Mkuu wa jimbo uliofanyika Desemba 26-29 mwaka jana, ni mamlaka ya juu kulingana na kifungu cha 9(a) cha katiba ya Kanisa la Moravian, lakini pia maazimio ya mkutano huo ndiyo ambayo sasa tunayatekeleza,” alisema Mchungaji Mwaiseje na kuongeza kuwa pia mkutano huo ulichagua wajumbe 11 wa Halmashauri Kuu ambao katiba inawatambua kama Bodi.

“Utekelezaji wa maagizo haya ni pamoja na kupanga safu za viongozi kuanzia katika mabaraza ya wazee wa Kanisa kwenye sharika mbalimbali, kwa vile ushahidi umedhihirisha kuwa wengine wamekuwa wakikaidi maagizo ya viongozi wa juu,” alisema.

Alisema kuwa kanisa hilo halitaki kuona mipango yake ya maendeleo ikiwekewa pingamizi na watu waumini ama wachungaji kwa hila, badala yake imefungua milango ili wenye hoja za msingi watoe mawazo kwa nia ya kuboresha.

“Kanisa la Moravian kazi yake kubwa ni huduma za kiroho na wala sio ulingo wa siasa, sasa kuna waumini na wachungaji ambao kwa sasa wanapandikiza mbegu za chuki na kuendeleza migogoro,” alisema Mchungaji Mwaiseje.

No comments:

Post a Comment