.

.

.

.

Thursday

Majina Bunge la Katiba:Maaskofu Pentekoste wampinga Rais Kikwete

Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste nchini (PCT), limedai kusikitishwa na kitendo cha Serikali kuwabagua katika uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba. 
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Askofu David Batenzi, alisema wao ni miongoni mwa taasisi kubwa za kidini iliyo wasilisha majina serikalini kama walivyoagizwa.
Alisema Serikali inapaswa kukomesha mara moja ubaguzi wa kidini nchini ambao kimsingi umekuwa ukigawa watu kwa makundi ukitawaliwa na siasa, udini na ukabila. 
Aliongeza kuwa, kama Serikali itaendelea kung'ang'ania msimamo wa kutaka wajumbe wa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste wasihusike Bunge hilo, wataitisha Mkutano Mkuu ambao utajumuisha Maaskofu wote nchi nzima.
Wengine ambao watahusika na mkutano huo ni mitume na wachungaji wote ili kutafakari kwa pamoja hatima ya kutengwa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuchukua hatua ili haki iweze kutendeka kwa vizazi vijavyo. 
"Katika kutafakari mwenendo wa uongozi wa Serikali tangu awamu ya kwanza hadi ya nne, tumeona kuna mfumo dume unaofanya ubaguzi wa makusudi kwa baadhi ya makundi ya kidini na kukumbatia makundi mengine ya kidini.
"Hali hii imesababisha makundi mengine kuporwa haki zao za msingi wanazotakiwa kupewa na Serikali...utafiti uliofanywa hivi karibuni, unaonesha hali ya udini, siasa na ukabila ambao unajitokeza sana katika nchi yetu," alisema.
Alisema ubaguzi huo hujitokeza hasa unapofika wakati wa kuamua masuala muhimu yenye manufaa kwa ajili ya nchi pamoja na vizazi vijavyo.
Askofu Batenzi alisema Kamati Kuu ya Utendaji ya PCT Taifa, katika kikao chake cha Desemba 5,2013, walichagua majina ya watu walioona wanafaa kuchaguliwa katika Bunge hilo, lakini hakuna hata mmoja aliyechaguliwa.
Aliongeza kuwa, si mara ya kwanza kwa Serikali kupuuza mapendekezo ya Wapentekoste bali imekuwa ikiwabagua kila yanapojitokeza masuala muhimu yanayohusu uwakilishi wa kidini katikaTaifa. 
"Kwa muda wa miongo miwili, Wapentekoste tumekuwa tukinyimwa haki na Serikali ikiwemo ya kushiriki katika mambo ya msingi ya kitaifa.
"Serikali haitushirikishi katika sherehe za kitaifa kama inavyofanyika kwa taasisi nyingine za kidini, maombi ya dua wakati Rais mteule anapoapishwa na kuwekewa masharti magumu ya vibali vya mikutano ya injili," alisema. 
Alisema pengine Serikali inaona Wapentekoste hawana sifa za kuchaguliwa katika Bunge hilo hivyo ikaamua kuteua majina ya wajumbe kutoka taasisi nyingine zikiwemo za Waislamu, Wakatoliki, Walutheri, wengine binafsi Tanzania Bara, Visiwani na kuwaacha wao.
"Baraza la Kiislamu wamepewa nafasi 10, Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (TEC) wajumbe watatu, Walutheri (CCT) wajumbe watano na wawili binafsi lakini PCT hakuna hata mmoja.
Kwa Upande wake, Mjumbe wa Baraza la Utendaji ambaye pia ni Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zakaria Kakobe, alisema wamechoshwa kubaguliwa na Serikali hivyo watasimama kutetea haki yao.

Source:Majira

No comments:

Post a Comment